TIMU ya Azam Veteran imezidi kufanya kweli kwenye michuano ya maveterani ya Azam Fresco Cup baada ya jioni ya leo kuishudhia kipigo kizito cha mabao 6-0 Mbagala ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Azam Veteren kwenye michuano hiyo baada ya kuilaza Simba mabao 3-2 kwenye mchezo wa ufunguzi uliopigwa wikiendi iliyopita.

Mshambuliaji hatari na nahodha wa timu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’ ndiye aliyekuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Mbagala baada ya kufunga mabao mawili sawa na Mussa Lumbi na Huzu Kajembe huku Salim Aziz ‘Mahrez’ akipiga jingine.

Kwa ushindi huo Azam Veteran imejihakikishia kufuzu kwa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo itakayofanyika Agosti 6 mwaka huu, lakini bado inadaiwa mchezo mmoja wa mwisho wa makundi utakaofanyika Jumamosi ijayo saa 12.30 jioni.

Mechi nyingine za mwisho za hatua ya makundi zitawahusisha Simba itakayocheza na Mbagala (saa 11.00 jioni) huku Julai 31 Yanga akipambana na Binslum (saa 11.00 jioni) na TFF watakaoumana na Chamazi (saa 12.30 jioni). 

Baada ya mechi hizo za makundi, hatua ya nusu fainali itafuatia kuanzia Agosti 6 mwaka huu kwa washindi wawili wa juu wa kila kundi kupita na kuunda timu nne, ambazo zitatengeneza mechi mbili.

Mechi ya kwanza itakuwa kati ya mshindi wa Kundi A na mshindi wa pili wa Kundi B huku mshindi wa kwanza wa Kundi B akikutana na msshindi wa pili wa Kundi A, ambapo mechi hizo zitahitimishwa kwa mchezo wa fainali utakaofanyika siku ya Sherehe ya Nane Nane (Agosti 8 mwaka huu).