KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imeendelea kujiandaa vilivyo kuelekea msimu ujao, ambapo leo asubuhi imeifunga Mshikamano mabao 5-0.

Mchezo huo wa tatu wa kirafiki wa kujipima ubavu umepigwa ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Kocha Mkuu Zeben Hernandez alipata fursa ya kuwatathimini wachezaji wake wote wakiwemo wanaofanya majaribio.

Mechi mbili za awali ambazo timu hiyo imeshinda ni zile dhidi ya Ashanti United iliyowachapa mabao 2-0 kabla ya kuwatandika Friends Rangers 2-1 Jumatano iliyopita.

Azam FC imeonekana kuimarika sana kwenye mchezo wa leo hasa kipindi cha kwanza, ikicheza soka la kueleweka la kasi, pasi fupi fupi na kukaba kwa nguvu pale wanapokuwa hawana mpira.

Mabao ya Azam FC katika mchezo huo yalifungwa na na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ dakika ya tatu, akitumia vema pasi ya Shaaban Idd, huku Mudathir Yahya akitupia la pili dakika ya sita kufuatia pasi ya Fuadi Ndayisenga.

Mudathir aliyetakata kwenye mchezo huo alifunga bao la tatu dakika ya 14 kwa shuti kali nje kidogo ya eneo la 18 kufuatia pasi safi ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shaaban alifunga hesabu za mabao za Azam FC katika kipindi cha kwanza kwa kufunga bao la nne dakika ya 44 akitumia vema pasi ya Bocco.

Kocha wa Azam FC, Zeben alibadilisha kikosi chote kilichoanza kipindi cha pili, ambacho safari hii kilisheheni wachezaji wengi vijana.

Kipindi cha pili kilionekana kwenda nguvu sawa kwa pande zote, lakini Azam FC ndio ilifanya mashambulizi makali langoni mwa Mshikamano na kufanikiwa kupata bao la tano dakika ya 88 likifungwa na Farid Mussa kwa shuti la kiufundi akimalizia pasi murua ya Gardiel Michael.

Baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho Jumapili kujiandaa na safari ya kuelekea Visiwani Zanzibar Jumatatu kuweka kambi ya kutafuta utulivu na kufanya maandalizi ya kiufundi zaidi kuelekea msimu ujao.

VIKOSI AZAM FC

First Half:

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Himid Mao ‘Ninja’, Jean Mugiraneza ‘Migi’, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor (C), Shaaban Idd, Fuadi Ndayisenga.

Second Half:

Metacha Mnata, Ismail Gambo ‘Kusi’, Gadiel Michael, Abdallah Kheri, David Mwantika, Abdallah Masoud ‘Cabaye’, Omary Wayne, Frank Domayo (C), Ramadhan Singano ‘Messi’/Farid Mussa, Rajab Odasi, Khamis Mcha ‘Vialli’