MICHUANO ya timu za maveteran ya Azam Fresco Cup, inatarajia kutimua tena vumbi wikiendi hii ambapo itashuhudiwa timu mwenyeji Azam Veteran ikisaka nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali kwa kukipiga na Mbagala Veteran keshokutwa Jumapili saa 9.30 alasiri.

Mchezo huo wa Kundi A utapigwa Uwanja wa Azam Complex, ambao utafuatiwa na mwingine kati ya TFF Veteran na Binslum Tyres utakaoanza kutimua vumbi kuanzia saa 11.00 jioni na ule wa funga dimba utawahusisha Yanga Veteran na Chamazi Veteran (saa 12.30 jioni).

Huo utakuwa ni mchezo wa pili wa Azam Veteran kwenye michuano hiyo, ambapo katika fungua dimba iliichapa Simba Veteran mabao 3-2 na ushindi wowote Jumapili ijayo utaifanya kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa hatua ya nusu fainali ikiwa kinara wa kundi lake.

Kabla ya mechi hizo za keshokutwa, burudani ya michuano hiyo itaendelea kesho Jumamosi kwa michezo miwili, wa kwanza ukiwakutanisha Yanga Veteran na TFF Veteran (saa 11.00 jioni), ambazo bado hazijacheza mechi zozote huku Simba Veteran ikifuatia kwa kuonyeshana kazi na Mbagala kuu Veteran (saa 12.30 jioni).

Michuano hiyo ya wiki tatu, itamalizia mzunguko wa kwanza wa hatua ya makundi wiki ijayo, kwa Simba kucheza na Mbagala (saa 11.00 jioni) na Azam kukipiga na Mbagala Kuu (saa 12.30 jioni), zote zikifanyika Julai 30 mwaka huu, huku zile za Julai 31 zikiwahusisha Yanga dhidi ya Binslum (saa 11.00 jioni) na TFF watakaoumana na Chamazi (saa 12.30 jioni).  

Baada ya mechi hizo za makundi, hatua ya nusu fainali itafuatia kuanzia Agosti 6 mwaka huu kwa washindi wawili wa juu wa kila kundi kupita na kuunda timu nne, ambazo zitatengeneza mechi mbili.

Mechi ya kwanza itakuwa kati ya mshindi wa Kundi A na mshindi wa pili wa Kundi B huku mshindi wa kwanza wa Kundi B akikutana na msshindi wa pili wa Kundi A, ambapo mechi hizo zitahitimishwa kwa mchezo wa fainali utakaofanyika siku ya Sherehe ya Nane Nane (Agosti 8 mwaka huu).