RATIBA ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu ujao imetoka rasmi jana huku Azam FC ikianza kampeni ya kufukuzia taji hilo kwa kuivaa African Lyon kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Agosti 20 mwaka huu.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) hivi sasa wameshaanza maandalizi ya msimu huo, ambapo wanafundishwa na makocha wapya kutoka nchini Hispania chini ya Kocha Mkuu Zeben Hernandez.

Moja ya mipango mikubwa aliyojiwekea Zeben msimu uliopita ni kuifanya Azam FC kuwa timu bora yenye kupata matokeo pamoja na kuwapa furaha mashabiki wake.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) inaonyesha kuwa Azam FC itacheza mechi saba tu nyumbani kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi na nane ugenini.

Azam FC iliyomaliza msimu uliopita ikishika nafasi ya pili, safari hii imepania vilivyo kurejesha taji lake la ligi walilotwaa msimu 2013/14 kwa rekodi ya kutofungwa mchezo wowote.

Hadi inamaliza msimu huo, Azam FC haikuweza kupoteza mchezo wowote ndani ya Uwanja wa Azam Complex, huku ikifunga jumla ya mabao 47 na kufungwa 24 na kuifanya kujihakikishia nafasi ya pili kwa pointi 64.