NI wazi sasa kipa wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aishi Manula, hana mpinzani miongoni mwa makipa wenzake nchini.

Unaweza kujiuliza maswali mengi na kushangaa, lakini ndio iko hivyo na hii ni baada ya usiku wa kuamkia leo Jumatatu kutwaa Tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Aishi ametwaa tuzo hiyo akiwabwaga Beno Kakolanya aliyekuwa Tanzania Prisons msimu uliopita hivi sasa akihamia Yanga pamoja na Deogratius Munishi ‘Dida’ (Yanga).

Tuzo hiyo inaifuatia ile aliyotwaa awali Mei 25 mwaka huu, ilipomalizika michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), alipotangazwa kuwa Kipa Bora wa michuano hiyo.

Hiyo ni rekodi ya aina yake kwa Aishi kwani kwa kutwaa tuzo zote za langoni msimu uliopita inamaanisha kuwa amewafunika makipa wote nchini wakiwemo baadhi ya wakongwe akiwa na umri mdogo wa miaka 21 tu.

Kwa mujibu wa takwimu, Aishi alicheza asilimia 99.7 ya mechi zote za Azam FC msimu uliopita zikiwemo za kirafiki, akidaka langoni dakika 4,628 (sawa na mechi 51 na dakika 38).

Asilimia 0.3 zilizobakia, kipa huyo aliwaachia waliokuwa wapinzani wake Ivo Mapunda na Mwadini Ally, waliodaka mechi chache za Azam FC msimu uliopita.

Kipa huyo aliyekuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, hadi anakuwa kipa bora wa VPL, amefanikiwa kudaka dakika 2,550 (sawa na mechi 28 na dakika 30) na hii akiwazidi wachezaji wote ndani ya ligi hiyo.

Katika dakika hizo alizocheza za ligi, Aishi hajafungwa bao lolote (cleensheet) ndani ya michezo 12 na hii akiwapita makipa wengine wote ndani ya ligi hiyo.

Mechi pekee ya ligi aliyokosa msimu uliopita ni ile ya Ndanda iliyofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, na Azam FC kushinda bao 1-0, bao la beki wa kulia mwenye kasi na uwezo wa kufunga mabao Shomari Kapombe.

Pia mechi nyingine ambayo alicheza kwa dakika chache ni ile timu hiyo ilipoichapa Majimaji 2-1 mjini Songea, ambapo alilazimika kutolewa nje dakika ya 30 baada ya kuumia mguu na nafasi yake kuchukuliwa na Mwadini Ally.

Aishi aliyeibuka akitokea kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC (Azam Academy), moja ya vitu adimu alivyoonyesha msimu uliopita ni uwezo wake wa kukosa mikwaju ya penalti na kuokoa michomo hatari langoni.

Baadhi ya penalti alizookoa ni zile alizoiongoza Azam FC kushinda dhidi ya Mwadui (1-0) aliyopiga Rashid Mwandawa, Kagera Sugar (2-0) mpigaji akiwa Salum Kanoni na ile ya Yanga iliyopigwa na Thabani Kamusoko, mechi iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.

Wakati Aishi akitwaa tuzo hiyo, nyota mwingine wa Azam FC inayodhaminiwa na Benki na NMB, Farid Mussa, yeye hakufanikiwa kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi baada ya waandaji wa tuzo hizo kumchagua Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ kutwaa tuzo hiyo.

Kwenye usiku wa tuzo hizo, Azam FC iliweza kukabidhiwa hundi ya Sh. milioni 40, iliyopokelewa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, hii ni baada ya mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) kushika nafasi ya pili kwenye ligi msimu uliopita.

Tuzo nyingine

Wengine waliotwaa tuzo hizo ni beki wa Yanga, Juma Abdul, aliyeibuka Mchezaji Bora wa michuano hiyo, mshambuliaji wa Simba Ibrahim Ajibu aliyetwaa tuzo ya Goli Bora la msimu, Amissi Tambwe (Yanga) alikabidhiwa zawadi yake ya Ufungaji Bora, Thabani Kamusoko (Yanga) akiwa Mchezaji Bora wa msimu na Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm akiwa Kocha Bora, huku Mtibwa Sugar ikiwa Timu Bora yenye nidhamu.