TIMU ya Azam Veteran imeanza vema kufukuzia taji la michuano ya Azam Fresco Cup baada ya kuwachapa maveterani wenzao wa Simba mabao 3-2 jioni ya leo.

Mchezo huo wa ufunguzi wa michuano hiyo inayofanyika Uwanja wa Azam Complex, ilishuhudiwa Azam Veteran ikinawiri kabisa na kuwachachafya vilivyo Simba.

Kikosi cha Azam Veteran kilichoanza leo kiliundwa na baadhi ya viongozi wa Azam FC, Makamu Mwenyekiti Nassor Idrissa ‘Father’, Ofisa Mtendaji Mkuu Saad Kawemba na Meneja Luckson Kakolaki.

Mashujaa wa Azam Veteran walikuwa ni Nahodha wa kikosi hicho Abdulkarim Amin ‘Popat’ aliyefunga bao moja, huku Mussa Lumbi akifunga mawili na Simba ikijipatia yao kupitia kwa Spia Mbwembwe na Masanja.

Michuano hiyo itakayoendelea kufanyika kila wikiendi Jumamosi na Jumapili, iliendelea kwa mchezo wa pili na kushuhudia Mbagala Kuu wakiichapa Mbagala mabao 2-1.

Patashika ya michuano hiyo imemalizika usiku huu kwa mchezo kati ya timu y Binslum na Chamazi, ulioisha kwa kutoshana nguvu ya mabao 2-2.

Michuano hiyo kuendelea Jumamosi ijayo Julai 23 mwaka huu kwa mechi tatu, itakayoanza saa 9.30 Alasiri itawahusisha Yanga Veteran itakayocheza na TFF, itafuatiwa na Simba Veteran dhidi ya Mbagala Kuu (saa 11:00 jioni).

Mchezo wa mwisho utawakutanisha wenyeji Azam Veteran watakaokipiga na Mbagala Veteran.