KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo mchana imempokea nyota wa Kimataifa wa Niger, Chicoto Mohamed, aliyekuja kufanya majaribio ya kujiunga na timu hiyo.

Beki huyo wa kati aliyetokea katika timu ya ASM Oran ya Algeria aliyochezea msimu uliopita, ametua na kupokelewa na Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd.

Mara baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl Nyerere (JNIA), Chicoto alisema kuwa anafuraha kubwa kupewa nafasi hiyo na Azam FC.

“Kitu cha kwanza ninafuraha kubwa kuwa Tanzania, kazi yangu imenifanya kuwa hapa, hivyo ninafuraha kuwa hapa kuonyesha kile nilichonacho,” alisema.

Chicoto, 27, anayechezea timu ya Taifa ya Niger, mbali na kucheza soka Algeria pia amewahi kukipiga Sporting Sahel SC ya kwao (2006-2011), Platinum Stars ya Afrika Kusini (2011-2012), AS Marsa ya Tunisia (2012-2013) na Coton Sports ya Cameroon (2013-2014).

Beki huyo mwenye mwili mkubwa na kasi aliyefuga rasta, anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kucheza mipira ya juu na chini na ubora kwenye ukabaji kwa mujibu wa wasifu wake.

Ujiuo wa Chicoto aliyezaliwa nchini Benin, ni sehemu ya jitihada za Uongozi wa Azam FC kwa kushirikiana na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Zeben Hernandez, kutaka kuboresha kikosi cha timu hiyo kwenye eneo la ulinzi na ushambuliaji.