MICHUANO ya Kombe la Azam Fresco inatarajia kuanza rasmi keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Moja ya timu zitakazoshiriki michuano hiyo inayodhaminiwa na kinywaji safi kabisa kipya cha Azam Fresco, ni waandaaji wa michuano hiyo Azam Veteran, zingine zikiwa ni Simba Veteran, Yanga Veteran, Bin Slum na TFF.

Kwa mujibu wa nahodha wa Azam Veteran, Abdulkarim Amin ‘Popat’, alisema kuwa michuano hiyo itahusisha timu za maveterani peke yake huku ikidumu kwa takribani wiki tatu.

“Mashindano haya ni ya maveterani pekee, yatachukua muda wa wiki tatu, kila wikiendi Jumamosi na Jumapili zitachezwa mechi tatu kwa siku moja,” alimalizia Popat.

Azam Veteran ni moja ya timu bora za maveterani kwa sasa, ikiwa inaundwa na wachezaji kadhaa ambao ni Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Nassor Idrissa, Meneja wa timu hiyo Luckson Kakolaki, Kocha wa Makipa, Idd Abubakar, Salim Aziz ‘Mahrez’, Philip Alando.