KIUNGO wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Jean Baptiste Mugiraneza, tayari ameanza kujifua nchini kwao Rwanda kuelekea msimu ujao huku akiwaambia mashabiki wa timu hiyo wategemee makubwa kutoka kwake 2016/17.

Migi alijiunga na Azam FC Julai mwaka jana akitokea APR ya kwao kwa usajili huru, ambapo amefanikiwa kuonyesha kiwango kizuri kwenye eneo la kiungo wa ukabaji akichangia mafanikio ya matajiri hao kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame Agosti mwaka jana.

Akizungumza na mtandao wa rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kutoka nchini humo, Migi alisema ameshaanza kujifua tokea Juni 19 mwaka huu akiwa na kikosi cha timu yake ya zamani ya APR.

“Namshukuru Mungu kwa sasa niko vizuri kabisa, tayari kwa kuanza mikikimikiki ya msimu ujao, nawaahidi mashabiki wa Azam FC watarajie mambo mazuri kutoka kwangu msimu ujao,” alisema.

Azoea mazingira soka Tanzania

Alisema kwa sasa akirejea nchini keshoutwa Alhamisi usiku kwa ajili ya kuanza msimu ujao atakuwa yuko vizuri kabisa huku akisisitiza kuwa hivi sasa ameshalizoea soka la Tanzania.

“Msimu uliopita nilipata shida sana kwenye soka la Tanzania, nimekutana na mazingira tofauti na wachezaji tofauti na pia ligi ya hapa ikiwa ngumu sana na viwanja vingi vikiwa havina bora, ila kwa sasa nimeshazoea na nimejiandaa kuonyesha makubwa zaidi tofauti na msimu uliopita,” alisema.

Kuhamishia mabao Azam FC

Migi mbali na kuwa na sifa ya ukabaji mzuri, pia yuko vizuri kwenye eneo la ufungaji mabao, ambapo amewahi kuzifungia mabao APR na timu yake ya Taifa ya Rwanda ‘Amavubi’, ambapo hivi karibuni aliiongoza timu hiyo kuichakaza Mauritius 5-0 huku yeye akitupia wavuni mabao mawili.

“Najua bado nina deni kubwa zaidi Azam FC, nimekuwa nikiifungia mabao Rwanda na pia huko nyuma nikifungia APR, lakini kwa timu yangu mpya ya Azam FC bado sijawaweza kuipa bao lolote, kama nilivyokuambia toka awali nimekutana na changamoto nyingi sana hapa za ugeni, naweza kusema kuwa msimu ujao nitajitahidi kuyahamisha mabao niliyokuwa nikifunga huko na kuja kuyafunga hapa,” alimalizia Migi.

Migi pamoja na wachezaji wengine wa Azam FC hivi sasa ndio wanamalizikia likizo ya wiki tano waliyopewa, ambapo itamalizika rasmi keshokutwa Alhamisi na Ijumaa ijayo Julai 1, 2016 wanatarajia kuanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao (2016/17).