KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imezidi kupiga hatua katika utoaji wa habari zake kwenye mitandao ya kijamii, na sasa muda mfupi ujao inatarajia kufikisha ‘likes’ 400,000 za mashabiki wa soka wanaotembelea ukurasa wake wa facebook ‘Azam FC’.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi kabisa cha Azam Cola, imekuwa na utaratibu mzuri wa kisasa wa kutoa taarifa zake mbalimbali kupitia vyanzo vyake rasmi vya mitandao, jambo ambalo limekuwa likiwavutia watu wengi ambao wamekuwa wakipata urahisi kupata taarifa zinazojiri kuhusu timu hiyo.

Hadi kufikia asubuhi hii tayari ‘likes’ kwenye ukurasa huo zimefikia watu 399,791, zikiwa zimebakia ‘likes’ 209 kutimia 400,000, likiwa ni ongezeko la watu 100,000 (likes) tokea Februari 18 mwaka huu ilipotimiza ‘likes’ 300,000 na ni miongoni mwa timu 10 bora barani Afrika zinazofuatiliwa na watu wengi zaidi mitandaoni.

Sasa imezidi kukimbiza timu zote za Afrika Mashariki na Kati na Magharibi, lakini inazidiwa na baadhi ya timu kutoka Afrika Kusini (Kaizer Chiefs, Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns) na nyingine kutoka Kaskazini ambazo ni za Tunisia Etoile du Sahel, Esperance na Club Africain pamoja na Al Ahly (9,740,020) na Zamalek (5,311,260) za Misri, zinazoongoza barani Afrika.

Timu pekee inayoifuatia Azam FC kutoka Afrika Mashariki na Kati ni mabingwa wa Kenya Gor Mahia, waliofikisha ‘likes’ 284,463.

Hii ni hatua nzuri kwetu kwani tunaamini ya kuwa kupitia idadi hiyo ya watu wanaotufuatilia, sasa habari zetu na mambo mbalimbali yanayoendelea Azam FC yatakuwa yanawafikia zaidi ya Mamilioni ya Watanzania na watu wengi zaidi wanaoishi nje ya Taifa hili.

Kutokana na mfumo huo wa kuendesha timu kisasa, mabingwa hao wamekuwa wakijizolea mashabiki kila kukicha jambo, ambalo linazidi kuimarisha mbio za kuwa moja ya timu kubwa Afrika baada ya kufanikiwa kuteka soka la Afrika Mashariki na Kati.

Uongozi wa timu hiyo unawaomba mashabiki na wadau wa mchezo huo kufuatilia mitandao rasmi ya klabu kwa ajili ya kuendelea kupata habari motomoto zitakazojiri na zinazoendelea kujiri ndani ya Azam FC na kukaa mkao wa kula kuelekea msimu ujao wa 2016-2017.