NYOTA sita wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC wamethibitishwa na mashabiki kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa timu hiyo msimu uliopita.

Azam FC ilianza rasmi mchakato wa kusaka mchezaji bora wa timu hiyo kwa msimu uliopita Jumatao iliyopita kwa kuwapa fursa mashabiki kuwapigia kura wachezaji, na watano bora watakaochaguliwa mara nyingi wataingia kwenye fainali.

Hadi kufikia jana Ijumaa saa 1.00 usiku, siku ya mwisho ya kupiga kura, jumla ya mashabiki 810 waliweza kupiga kura kati ya kura hizo 200 ziliharibika kwa wapigaji kura kukiuka vigezo na masharti ya zoezi hilo.

Wachezaji walioingia kwenye fainali hiyo ni beki wa kulia Shomari Kapombe, aliyeoongoza kupigiwa kura nyingi akipata 277 na kufuatiwa na kipa namba moja Aishi Manula (120) pamoja na wengine beki Pascal Wawa (40), kiungo Himid Mao ‘Ninja’ (30) huku Farid Mussa na Ramadhan Singano ‘Messi’ wakifunga dimba kwa kulingana kura kila mmoja akiwa nazo 27.

Kura nyingine 89 zilizobakia wamegawana wachezaji kadhaa akiwemo nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Kipre Tchetche, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Khamis Mcha, Erasto Nyoni, Abdallah Kheri, Shaaban Idd, Ivo Mapunda, Allan Wanga, Didier Kavumbagu na Aggrey Morris.

Zoezi hilo la fainali limehusisha nyota sita badala ya watano kutokana na kulingana kura kwa Farid na Singano.

Zoezi hilo la kupiga kura kwa hatua hiyo ya fainali kabla ya kumpata mshindi, litaanza rasmi leo Jumamosi na litadumu hadi Jumatano ijayo Juni 15 mwaka huu saa 6.00 mchana na mshindi atatangazwa rasmi.

Uongozi wa Azam FC utatoa rasmi tuzo hiyo kwa mchezaji husika kwenye mchezo wa kwanza wa Azam FC msimu ujao itakapocheza nyumbani.