Nani kuibuka mchezaji bora wa Azam FC 2015/16?

NI wiki mbili sasa zimepita tokea msimu wa 2015/16 umalizike, sasa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, inakupa fursa shabiki wa timu hiyo kumchagua Mchezaji Bora wa Azam FC msimu uliopita.

Itakumbukwa kuwa Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, moja ya mafanikio yake msimu uliopita ni kutwaa ubingwa wa kwanza wa michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), ikashika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC pia ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano maalumu ya timu nne iliyofanyika nchini Zambia Januari mwaka huu huku pia ikiwa washindi wa pili kwenye Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Mchezaji Bora atakuwa ni yule aliyepigiwa kura nyingi na mashabiki na atajishindia tuzo maalumu itakayoandaliwa na uongozi wa mabingwa hao.

Tuzo hiyo itakabidhiwa kwa mchezaji husika kabla ya kuanza kwa mchezo wa kwanza wa Azam FC, itakayocheza nyumbani msimu ujao.

Hivyo ni wakati wako ewe shabiki wa Azam FC kumpendekeza mchezaji aliyekufurahisha msimu uliopita kutokana na kiwango chake bora, na unaona anastahili kuwa mchezaji bora wa msimu wa timu hiyo.

Zoezi la kumpendekeza mchezaji husika litaanza leo na kudumu hadi Ijumaa saa 1.00 usiku, baada ya hapo wachezaji watano waliopata kura nyingi watakaingizwa kwenye fainali ya kumpata bingwa atakayekuwa amejizolea kura nyingi zaidi kutoka kwa mashabiki.

Mashabiki wataanza tena kupiga kura kwa hatua hiyo ya fainali kuanzia Jumamosi hadi Jumatano ijayo Juni 15 mwaka huu saa 6.00 mchana na baada ya hapo mshindi wa tuzo hiyo atakayekuwa na kura nyingi atakuwa amepatikana.

Mashabiki nao kuzawadiwa

Kutokana na mashabiki wengi kuiunga mkono vema timu hiyo kwa msimu wote uliopita hadi unamalizika, uongozi wa Azam FC utawazawadia mashabiki 10 jezi za timu hiyo, ambao watakuwa wameshiriki kikamilifu kwenye zoezi hili pamoja na wale waliokuwa wakichangia ipasavyo katika ukurasa rasmi klabu ndani ya mtandao wa kijamii wa facebook uitwao ‘Azam FC’.  

Mashabiki pekee watakaozingatiwa kwenye na kujizolea jezi hizo ni wale waliou-like ukurasa huo, ambao hivi sasa unakaribia kufikisha ‘like’s’ laki nne (400,000) ukiwa umebakiza takribani ‘like’s’ 8,770 hadi kufikia mchana huu leo Jumatano.

Vigezo na masharti kwa wapiga kura;

*Shabiki hataruhusiwa kupiga kura zaidi ya moja ndani ya zoezi moja, atakayefanya hivyo kura yake itakuwa imeharibika.

*Kwa shabiki yoyote atakayeonyesha kumpigia kampeni mchezaji yoyote ili kuwashawishi wengine wampigie kura, kura yake itakuwa imeharibika na pia atakakuwa amejiondoa kwenye mchakato mzima.

*Hakuna kura itakayohesabiwa baada ya muda rasmi wa kupiga kura kwenye zoezi husika kuisha.