TUZO za michuano ya Azam Youth Cup 2016, walizotwaa nyota wa timu ya vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ‘Azam FC Academy’, Shaaban Idd na Abbas Kapombe, zimewakumbusha vitu vikubwa ndani ya maisha yao ya soka.

Wakati Azam FC Academy ikiibuka mabingwa wa michuano hiyo mbele ya timu nyingine tatu shiriki Football for Good Academy (Uganda), Ligi Ndogo Academy (Kenya) na Future Stars Academy (Arusha), Kapombe alitwaa Tuzo ya Beki Bora na Shaaban Idd, akitwaa Tuzo ya Mshambuliaji Bora na Mfungaji Bora.

Wakizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kwa nyakati tofauti mara baada ya kumalizika michuano hiyo, walisema tuzo hizo zimewafungulia milango ya kuongeza bidii na kufanya vizuri zaidi ili kufikia mafanikio.

“Namshukuru Mungu kwa kunifanikishia malengo yangu, nahisi ndio njia yangu ya kwanza kanifungulia kwa ajili ya kufanya vizuri mbeleni, hapa tumekutana na timu nyingi zenye ushindani hususani timu hii ya Uganda (Football for Good), wametupa changamoto fulani hivi, japo tumewafunga lakini wametupa tabu sana kwa soka lao pasi,” alisema.

Kapombe alisema kuwa tuzo aliyopata inamaanisha kitu kikubwa kwake kuwa aongeze bidii na kufika mbali zaidi pamoja na kutobweteka baada ya mafanikio hayo.

Shaaban Idd naye anena

Kwa upande wake Shaaban Idd alisema kuwa anafuraha kubwa mara baada ya kutwaa tuzo hiyo huku akisisitiza kuwa ni njia yake ya kwanza ya kufikia mafanikio makubwa zaidi kuanzia msimu ujao.

“Katika siku ambayo nina furaha kubwa kwenye maisha yangu basi ni leo (jana), nina furaha sana kutwaa tuzo mbili na hii ilikuwa mipango yangu kwani kabla hatujaanza hii michuano maandalizi yangu yalikuwa ni makubwa kwa ajili ya kupata kitu fulani, hivyo namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifanikishia kupata tuzo hizi,” alisema.

Shaaban alisema kuwa hatoishia hapo baada ya kupata mafanikio hayo bali ataendeleza moto zaidi kadiri ninavyoweza na namuomba Mwenyezi Mungu anisapoti kwenye hilo.

“Tuzo hizi nazipeleka kwa Wazazi wangu wote wawili na familia kwa ujumla kwani wao ndio wamenilea mpaka leo,” alisema.

Mshambuliaji huyo alipandishwa kwenye kikosi cha wakubwa mwishoni mwa msimu uliopita kufuatia kiwango chake bora anachoendelea kuonyesha katika mechi za Azam Academy, akisifika kwa mashuti, uwezo mkubwa wa kufunga mabao, kupambana na mabeki kutokana na umbile lake kubwa pamoja na uwezo mwingine wa kuruka hewani na kupiga mipira ya vichwa.