MKUU wa Maendeleo wa kituo cha kukuza vipaji cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ‘Azam FC Academy’, Tom Legg, amesifu kiwango kilichoonyeshwa na vijana wake kwenye mchezo wa jana dhidi ya Football for Good Academy huku akichukizwa na kadi nyekundu aliyopata nahodha wake Abdallah Masoud ‘Cabaye’.

Azam FC Academy imeendeleza wimbi lake la ushindi mnono kwenye michuano ya vijana ya Azam Youth Cup 2016 inayoendelea ndani ya Uwanja wa Azam Complex baada ya jana kuichapa timu hiyo kutoka Uganda mabao 5-1.

Ushindi huo umeifanya timu hiyo kufikisha jumla ya pointi sita ikiwa kinara wa ligi hiyo, na imejiwekea asilimia 98% za kutwaa ubingwa huo ikihitaji sare tu katika mchezo wa mwisho wa kesho Jumapili dhidi ya Ligi Ndogo Academy kutoka nchini Kenya itakayoanza saa 1.00 usiku.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Legg alisema kuwa kadi nyekundu aliyoipata nahodha huyo dakika ya 87 ni ya kizembe ikizingatiwa walikuwa wakiongoza kwa ushindi mnono wa mabao 5-1.

“Nimehuzunishwa sana kwa nahodha wetu kupata kadi nyekundu, kwa nahodha wetu kupata kadi nyekundu dakika chache kabla ya mpira kumalizika huku tukiwa tunaongoza mabao matano imeonyesha namna gani kuwa hajapevuka aliyoonyesha utoto, hasa kwa mchezaji ambaye anatakiwa kuwa katika kikosi cha kwanza, amekuwa kiongozi mbaya katika mchezo huo akiwa kama nahodha,” alisema.

Legg alichukua fursa kuwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo mnono, akisema kuwa ni mfululizo wa kiwango kizuri kwa timu yake tokea walipoanza mchezo wa kwanza kwa kuifunga Future Stars Academy mabao 4-1 Jumatano iliyopita.

“Nimefurahishwa na kiwango cha timu yangu kipindi cha kwanza tulikimili kwa asilimia kubwa na kushinda 4-0, tulicheza kwa nguvu, kasi na kwa kuonana vema, lakini kipindi cha pili tulishuka kidogo na mchezo kuwa nguvu sawa na hata matokeo yalikuwa 1-1, mpaka sasa nimefurahishwa na namna timu yangu inavyocheza hii michuano na kwa nafasi tuliyopo tunastahili na nasubiria mchezo wa mwisho kujua tutafanya nini,” alisema.

Kocha huyo raia wa Uingereza alisema kupitia michuano hiyo hawaangalii tu kutwaa ubingwa huo bali kujifunza namna ya kuandaa michuano ili baadaye kuiongeza zaidi timu na kuongeza ushindani zaidi huku akisema kuwa mpaka sasa ameridhishwa kwa namna michuano hiyo inayofanyika na ushindani unaoonyeshwa na timu zote.

Michuano hiyo leo Jumamosi inaingia kwenye mapumziko kwa timu zote shiriki (Azam Academy, Football for Good Academy, Future Stars Academy na Ligi Ndogo Academy) kwenda kushuhudia mchezo wa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kati ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na Misri itayofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.