WAKATI leo zikitarajiwa kuchezwa mechi za pili za michuano ya vijana ya Azam Youth Cup 2016, mchuano mkali umeibuka kwa wachezaji wanaowania ufungaji bora wa michuano hiyo.

Leo michuano hiyo itaendelea kwa wenyeji Azam FC Academy kucheza na Football for Good Academy kutoka Uganda (saa 1.00 usiku) huku mchezo utakaotangulia saa 10.00 jioni ukiwahusisha Ligi Ndogo Planet Academy (Kenya) dhidi ya Future Stars Academy (Arusha).

Mchuano huo mkali kwa wapachika mabao uko baina ya wachezaji watatu tofauti waliofunga mabao mawili kila mmoja kwenye mechi za awali, ambao ndio wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo ya kiatu cha ufungaji bora.

Azam FC Academy iliyoshinda mabao 4-1 kwenye mchezo wa awali dhidi ya Future Stars, imetoa wachezaji wawili katika chati hiyo ambao ni mshambuliaji hatari Shaaban Idd na kiungo fundi Rajabu Odasi, kila mmoja akiwa amepachika mabao mawili.

Mchezaji mwingine anayekamilisha orodha hiyo ni mshambuliaji hatari wa Ligi Ndogo Planet Academy, Eric Kivuva, aliyepachika mabao mawili yaliyoipa ushindi wa mabao 2-1 timu yake dhidi ya Football for Good Academy katika mchezo uliokuwa mkali na wa aina yake.

Mshambuliaji wa Football for Good, Otim Dradiga na kiungo Nazir Abdul kutoka Future Stars, wenyewe wanakamilisha idadi ya mabao nane yaliyofungwa mpaka sasa kwenye mechi mbili zilizofanyika za michuano hiyo, kila mmoja akiwa amefunga bao moja yakiwa ya kufutia machozi kwa timu zao.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mshambuliaji wa Azam FC Academy, Shaaban Idd, alisema amejipanga vilivyo kuondoka na tuzo hiyo ya ufungaji bora.

“Namshukuru Mungu mpaka sasa hivi tumefanikiwa kucheza mechi ya mwanzo na nimefunga mabao mawili, sitoishia mabao mawili tu nataka mechi mbili hizi zilizobakia niongeze mabao mengine zaidi ikiwezekana nifikie mabao saba, nane na kuweza kuchukua ufungaji bora katika ligi hii ndogo,” alisema.

Idd alisema anajua kuwa ana changamoto ya kupambana na wachezaji wengine wawili katika vita hiyo, lakini amedai atajitahidi kadiri iwezekanavyo kuongeza ujuzi zaidi kwa kushirikiana na wenzake na kutimiza ndoto yake hiyo ya kutwaa kiatu hicho.

Mbali na mfungaji bora kupewa tuzo maalumu, pia tuzo zingine za michuano hiyo zitakuwa kwa bingwa kuondoka na kombe, pamoja tuzo binafsi kwa wachezaji katika kila idara (kipa, beki, kiungo, mshambuliaji) bila kusahau tuzo ya mchezaji bora wa Azam Youth Cup 2016.