TIMU ya vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ‘Azam FC Academy’ sasa ina asilimia 98 za kutwaa ubingwa wa michuano ya Azam Youth Cup 2016.

Hiyo inatokana na timu hiyo kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Football for Good Academy ya Uganda katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex usiku wa leo.

Ushindi huo umeifanya Azam FC Academy kufikisha jumla ya pointi sita baada ya ushindi wa mechi zote mbili ilizocheza za michuano hiyo, ya kwanza wakianza kuichapa Future Stars Academy mabao 4-1.

Future Stars iliyoichapa Ligi Ndogo Academy mabao 3-1 kwenye mchezo wa awali saa 10.00 jioni, ushindi wao huo umewapunguza kasi Wakenya katika mbio za ubingwa kwani mpaka sasa timu hizo zote zimelingana kwa pointi, kila mmoja akijikusanyia tatu.

Hiyo inamaanisha ya kuwa wakati timu zote zikiwa zimebakisha mchezo mmoja, Azam FC Academy sasa inahitaji sare yoyote kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Ligi Ndogo keshokutwa Jumapili saa 1.00 usiku ili kutwaa ubingwa huo kwani itafikisha pointi saba ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

Hata ikifungwa kwenye mchezo wa mwisho, ili ikose ubingwa huo itazilazimu Future Stars na Ligi Ndogo zinazomfuatia zishinde mechi zao za mwisho kwa wastani wa mabao  8-0, yaani Ligi Ndogo iifunge Azam Academy (8-0) na Future Stars iichape Football for Good (8-0).

Iliichukua dakika 13 za mwanzo tu kwa Azam Academy kuweza kupata mabao matatu ya haraka, yaliyofungwa na Yahaya Zaidi dakika tano na 13 pamoja na Shaaban Idd katika dakika ya tisa, mabao yaliyowavuruga vijana wa Football for Good na kutoka mchezoni.

Yahaya aliingia kwenye vitabu vya rekodi ya michuano hiyo baada ya kufunga hat-trick ya kwanza katika dakika ya 39 akiifungia bao la nne Azam FC Academy na kufanya mpira kwenda mapumziko kwa uongozi wao wa mabao 4-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC Academy kuendeleza kasi yao ya mshambulizi na hatimaye ikahitimisha ushindi wake mnono kwa kupata bao la tano dakika ya 48, lililofungwa na nahodha wake kiungo Abdallah Masoud ‘Cabaye’.

Football for Good iliamka na kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa mshambuliaji wake hatari Dradiga Otim akitumia vema uzembe wa safu ya ulinzi wa kati ya Azam FC Academy.

Azam FC Academy ilipata pigo dakika ya 87 baada ya Masoud kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kuwa nyekundu kwa kumchezea madhambi Ganukura Allan na hivyo kumaliza mchezo huo wakiwa pungufu.

Future Stars yaionyesha Ligi Ndogo

Future Stars iliyoanza michuano hiyo kwa kupokea kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Azam Academy, leo imezinduka baada ya kuonyesha kandanda safi na kuichapa Ligi Ndogo mabao 3-1.

Kiungo Mahmudu Said ndiye aliyeibuka nyota wa mchezo huo baada ya kutupia mabao mawili mwenyewe kwa ufundi mkubwa, la kwanza akifunga kwa mkwaju wa moja kwa moja wa adhabu ndogo dakika ya 46 na jingine dakika ya 71 kwa shuti nje kidogo ya eneo la 18.

Bao jingine la Future Stars lilifugwa na Ramadhan Soloka dakika ya 18 huku Remy Sheikh akifunga bao pekee la Ligi Ndogo kwa mkwaju wa penalti dakika ya 37 kufuatia Baraka Fredi kumwangusha ndani ya eneo la hatari Isaac Ochieng

Michuano hiyo kesho Jumamosi itaingia kwenye mapumziko, ambapo timu zote zitaenda kushuhudia mchezo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ dhidi ya Misri, utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 Vikosi vilivyokuwa leo:

Azam Academy: Metacha Mnata, Abdul Omary, Ramadhan Mohamed, Abas Kapombe, Adolph Mtasigwa, Prosper Mushi/Joshua John dk 75, Yahaya Zaidi/Sadalla Mohamed dk 75, Masoud Abdallah, Shaaban Idd/Kolongo Idd dk 81, Rajabu Odasi, Fereji Salum/Optatus Lupekenya dk 59

Football for Good: Abraham Opio/Desmond Arop dk 67, Justin Opiro/Peter Ouma dk 56, Geoffrey Cankura, Rogers Atube, Joel Akaka, Isaac Bradbury/Pixy Akena dk 56, Stephen Bongomin, Allan Ganukura (C), Derick Ocan, Dradiga Otim/Yona Opio dk 74, Dickens Kilama