MKUU wa Maendeleo wa kituo cha kukuza vipaji cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ‘Azam FC Academy’, Tom Legg, ameanza kuijenga na kuipa mbinu za kimchezo timu hiyo kupitia michuano ya Azam Youth Cup 2016.

Michuano hiyo inaendelea kutimua vumbi ndani ya Uwanja wa Azam Complex, ambapo Azam FC Academy iliianza vema kwa kuichapa Future Stars Academy mabao 4-1 jana na kesho saa 1.00 usiku itashuka tena dimbani kupambana na Football for Good ya Uganda.

Legg ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa michuano hiyo ni maalumu kwa vijana wake kujifunza namna ya kucheza kwa namna tofauti ndani ya mchezo huku akidai kuwa wamefanikiwa kwenye hilo kwa asilimia kubwa katika mchezo huo wa kwanza.

“Ni jambo la kufurahisha kushinda mchezo wa kwanza, ni matokeo mazuri kwetu, nimeridhishwa sana namna tulivyocheza kipindi cha kwanza, tulicheza kwa nguvu sana na kupata mabao, tulipokuwa na mpira tulishambulia kwa haraka, kipindi cha pili tuliingia na mipango mingine kabisa ya kuumiliki mchezo, tukiwa tunaongoza mabao 4-1 hakutakiwa tuende tena kupambana nao kwa namna tulivyocheza kipindi cha kwanza.

“Nilitaka tujifunze namna ya kuumiliki mchezo pale tunapoongoza, hatukuwaachia nafasi ya wao kufanya mashambulizi ya kushutukiza, hata ya kupiga mashuti yaliyolenga lango letu kama walivyofanya kipindi cha kwanza wakati tunatafuta mabao, na hiyo yote tuliiweza kutokana na sisi kuumiliki mchezo huo,” alisema.   

Alisema ameridhishwa mno na kiwango cha wachezaji wake huku akidai kuwa wamejipanga kuendeleza ubora na kupambana katika mechi zote ikiwemo kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

“Kwanza tunatakiwa kufanya vema kwenye michuano hii na kuchukua kombe, lakini wakati huo huo tunatakiwa kukumbuka kuwa tunatakiwa kujifunza, kwangu mimi nathubutu kusema kuwa tumeweza kuonyesha kucheza kwa namna tofauti, kipindi cha kwanza tukicheza kwa nguvu, mbinu, kupambana, kupeleka mbele mpira kwa haraka ili kupata mabao, na kipindi cha pili tumejaribu kuja na mbinu ya kumiliki mpira zaidi ili kuulinda ushindi,” alisema.

Wachezaji wa Azam FC Academy walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kushika mafunzo hayo na hatimaye ikaweza kuondoka na ushindi huo mnono na kumiliki mpira katika vipindi vyote viwili.    

Tumeshuhudia msimu huu namna timu ya wakubwa ya Azam FC ilivyokuwa ikishindwa kulinda mabao wanayopata kipindi cha kwanza kwa kuipa mwanya timu pinzani kusawazisha mabao kipindi cha pili hasa kwa kushindwa kuumiliki mchezo kipindi hicho.

Azam Academy vs FFG

Ushindi wowote wa Azam Academy dhidi ya Football for Good ya Uganda kesho Ijumaa utaifanya kuukaribia ubingwa wa michuano hiyo kwani itafikisha jumla ya pointi sita na kuwaondoa kwenye mbio hizo Waganda hao.

Mchezo mwingine utakaotangulia saa 10.00 jioni utawahusisha Future Stars Academy kutoka Arusha ambao hawana pointi yoyote kama FFG, aambao wataumana na Ligi Ndogo Academy kutoka Kenya yenye pointi tatu walizozipata baada ya kuichapa FFG mabao 2-1.