ILIKUWA imebakia wiki, ikaja siku kadhaa, lakini hivi sasa zimebakia saa kadhaa kabla ya kuanza kwa michuano ya vijana ya Azam Youth Cup inayoandaliwa na Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC.

Michuano hiyo ya vijana ambayo ni ya aina yake itakayohusisha timu nne kutoka nchi tatu za Afrika Mashariki, itaanza kutimua vumbi ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia kesho (Juni 1) saa 10.00 jioni hadi Juni 5 itakapohitimika.

Wenyeji wa michuano hiyo Azam Academy ndio watakaonza kufungua michuano hiyo kwa kuvaana na Future Stars Academy kutoka mkoani Arusha, mechi itakayoanza saa 10.00 jioni.

Mechi nyingine itakayofuatia kuanzia saa 1.00 usiku, itakuwa ni baina ya waalikwa wa michuano hiyo kutoka nje ya nchi, Ligi Ndogo Academy (Kenya) watakaoonyeshana kazi na Football for Good Academy inayotokea nchini Uganda.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuelekea kwenye mchezo wa kesho, Kocha Msaidizi wa Azam Academy, Idd Cheche, alisema kuwa lengo lao kubwa ni kufanya vizuri kwenye michuano hiyo kwa kushinda mechi wanazocheza na hatimaye kuibuka mabingwa.

“Ni muda mrefu sasa vijana wetu hawajapata fursa ya kucheza mechi za kimashindano, hivyo michuano hii itawasaidia kuonekana, malengo yetu makubwa kwanza ni kuwapa fursa vijana kuonyesha uwezo wao na pia kushindana

“Pia tumedhamiria kuchukua ubingwa wa michuano hiyo kwa kushinda kila mechi tutakazocheza, haiwezekani kabisa tuzialike timu, zije hapa tuzihudumie, tuwape kila kitu, halafu na kombe nalo wachukue hapa hapa kwenye uwanja wetu hii itakuwa si vizuri, nia yetu kubwa ni kufanya vizuri,” alisema.

Baadhi ya mastaa wa Azam Academy wanaotarajiwa kuonekana kwenye michuano hiyo ni mshambuliaji hatari Shaaban Idd, kiungo Abdallah Masoud ‘Cabaye’, ambao mwishoni mwa msimu huu walipandishwa kwenye kikosi timu kubwa ya Azam FC.

Wengine watakaoonekana ni Mohamed Sadallah, Optatus Lupekenya, Yohana Nkomola, Yahaya Zaid, Fereij Salum, Rajabu Odasi, Abbas Kapombe.     

Michuano hiyo itakuwa ikiendeshwa kwa mfumo wa ligi, ambapo bingwa atakuwa ni yule atakayekusanya pointi nyingi baada ya kucheza mechi moja moja za wenyewe kwa wenyewe.

Hakutakuwa na kiingilio chochote watakachotozwa mashabiki watakaokuja kuhudhuria michuano hiyo, hivyo mashabiki wanaombwa kuhudhuria kwa wingi kushuhudia burudani safi ya soka vijana na kwa wale watakaokuwa mbali na mkoa wa Dar es Salaam, basi watashuhudia uhondo wote kupitia kingamuzi cha Azam TV.

Hii ni mara ya kwanza kwa Azam FC kuandaa michuano hiyo, ambayo itakuwa endelevu kwa kufanyika kila mwaka ambapo kwa kuanzia imeanza na timu hizo nne na hapo baadaye itatanuliwa zaidi na kuhusisha timu nyingi zaidi.

Azam FC inayodhamini na Benki ya NMB ni moja ya timu za vijana endelevu zinazofanya mazoezi kila siku na academy yake imetoa wachezaji wengi waliosambaa kwa sasa nchini na wengine wakitamba kama vile nyota wa Yanga, Simon Msuva, beki wa kushoto wa Simba Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Ili kuiongezea makali academy yake, Novemba mwaka jana Azam FC iliamua kumuajiri Mkuu wa Maendeleo wa kituo hicho kutoka nchini Uingereza, ambaye ni Kocha Tom Legg, ambaye ni mtaalamu wa soka la vijana.