WACHEZAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, hivi sasa wapo kwenye mapumziko wa wiki tano hadi Juni 30, mwaka huu baada ya kumalizika kwa msimu wa 2015/16.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki bora kabisa kwa sasa nchini ya NMB, imemaliza msimu ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) nyuma ya ya mabingwa Yanga ikiwa na pointi 64.

Mabingwa hao pia wameshika nafasi ya pili katika Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kufungwa na Yanga mabao 3-1 kwenye fainali iliyofanyika Jumatano iliyopita ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wakati msimu huu ukiwa umemalizika yafuatayo ni baadhi ya matukio ya Azam FC katika namba, yakihusisha mechi zote walizocheza kuanzia za kirafiki na za mashindano yote waliyoshiriki:-     

1: Namba hii inawakilisha taji la kwanza la michuano ya Kombe la Kagame ililobeba Azam FC kihistoria tokea ilipoanzishwa mwaka 2007, ikiichapa Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 Agosti 2, 2015.

64: Idadi ya mechi ambazo Azam FC imecheza msimu huu, ikihusisha mechi za kirafiki na za mashindano.

4628: Hii inasimama badala ya kipa namba moja wa Azam FC, Aishi Manula, aliyeweka rekodi ya kucheza mechi nyingi kuliko mchezaji yoyote wa timu hiyo, akicheza kwa dakika 4628 huku akitwaa tuzo ya Kipa Bora wa FA Cup. Rekodi hii pia inaweza kusimama kwa wachezaji wa timu nyingine.   

25: Hii inawakilisha mfungaji bora wa msimu wa Azam FC, Kipre Tchetche, aliyefunga mabao 25 kwenye mechi zote za Azam FC msimu huu.

10: Hii inamuhusisha kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, aliyetoa pasi nyingi za mwisho msimu huu ndani ya timu hiyo, ambapo amepiga 10.

8: Ni idadi ya mabao aliyofunga mmoja ya wachezaji wadogo kabisa kwenye kikosi cha Azam FC msimu huu, winga wa kushoto, Farid Mussa (20) ambaye huvalia jezi namba 17.

40: Hizi ni idadi ya mechi zote ambazo Azam FC imeshinda msimu huu tokea ilipoanza maandalizi Julai mwaka jana hadi ilipofunga msimu Mei 25 mwaka huu.

7: Mei 25 mwaka huu Azam FC ilifikisha idadi ya mechi saba ilizopoteza msimu huu, baada ya kufungwa kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Yanga mabao 3-1.

17: Sare ya bao 1-1 iliyoipata kwenye mchezo wa mwisho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mgambo JKT imeifanya Azam FC kumaliza msimu ikiwa imetoa sare 17 katika mechi zote.

113: Bao la mwisho la msimu alilofunga mshambuliaji Didier Kavumbagu kwenye fainali ya FA Cup, limeifanya Azam FC kumaliza msimu ikiwa imefunga jumla ya mabao 113.

180: Hizi ni dakika alizocheza kipa wa Azam FC, Ivo Mapunda, zikiwa ni chache kuliko mchezaji mwingine yoyote ndani ya timu hiyo msimu huu.

44: Bao la tatu ililofungwa Azam FC kwenye fainali ya FA Cup na winga wa Yanga Deus Kaseke, limeifanya timu hiyo kumaliza msimu ikiwa imeruhusu wavu wake kuguswa mara 44.

5: Inawakilisha ushindi mnono wa Azam FC msimu huu kwenye mechi rasmi za mashindano, iliifunga Toto Africans mabao 5-0 katika mchezo wa ligi Novemba 1, 2015 (Azam Complex).

12: Hii inasimama badala ya mchezaji Shomari Kapombe, aliyeweka rekodi ya kufunga jumla ya mabao 12 msimu huu akiwa kama beki wa kulia, akiwazidi mabeki wote wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL). Pia ndiye mchezaji pekee wa Azam FC aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi kwenye ligi msimu huu akichukua ya mwezi Januari mwaka huu.

114:  Hizi ni siku alizotumia beki Aggrey Morris, kukaa nje ya dimba akiuguza majeraha ya goti aliyopata wakati wa maandalizi ya kushiriki Kombe la Chalenji nchini Ethiopia Novemba mwaka jana akiwa na timu yake ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’. Alirejea dimbani kwa mara ya kwanza Machi 12 mwaka huu na kuiongoza Azam FC kuichapa Bidvest Wits mabao 3-0 jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

24: Hii inawakilisha tarehe 24 ya mwezi huu (Mei 24, 2016), siku ambayo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alizindua rasmi duka kubwa la vifaa vya michezo la timu hiyo ‘Azam Sports Shop’ lililopo Mtaa wa Swahili na Mkunguni, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, licha ya kufunguliwa duka hilo tayari lilianza kufanya kazi tokea Novemba mwaka jana likiuza baadhi ya vifaa vyenye nembo ya timu hiyo zikiwemo jezi, fulana, skafu, bendera, taulo, mipira, soksi, raba za michezo, mabegi ya mgongoni na kusukuma.

4: Ushindi wa mabao 2-1 iliyoupata Azam FC dhidi ya Esperance ya Tunisia kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, umeifanya timu hiyo kuandika rekodi ya kutofungwa mchezo wowote katika mechi nne ilizocheza za Kimataifa ndani ya uwanja wake wa nyumbani (Azam Complex). Nyingine ilizoshinda ni dhidi ya Bidvest Wits (4-3), El Merreikh (2-0) na Ferroviario Beira (1-0).

21: Ni rekodi waliyoiweka Azam FC msimu ya kucheza mechi 21 za mashindano mbalimbali bila kufungwa mchezo hata mmoja tokea Julai 19 walipoifunga KCCA (1-0) katika Kombe la Kagame hadi Januari 7 mwaka huu ilipofungwa kwa mara ya kwanza na Mafunzo (2-1) ndani ya michuano ya Mapinduzi Cup.

40: Hii inawakilisha zawadi ya fedha watakayopewa Azam FC na wadhamini Kampuni ya Vodacom kwa kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ambayo ni Sh. milioni 40.