KIPA namba moja wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aishi Manula, ameishukuru klabu hiyo kutokana na mafanikio anayoendelea kuyapata hivi sasa.

Aishi ametoa kauli hiyo kwenye ukurasa wa akaunti yake ya facebook kufuatia kumaliza msimu huu kwa kutwaa tuzo ya Kipa Bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

“Kwanza namshukuru Mungu kwa kunipa afya njema na kumaliza msimu huu vizuri.
Pia namshukuru kocha Idd Aboubakar (Kocha wa Makipa Azam FC) kwa kazi nzuri aliyofanya, pia niwashukuru magolikipa wenzangu Ivo Mapunda, Mwadini Ally, Metacha Mnata, Kauju kwa kuishi vyema na kusaidiana pamoja na kushirikiana tukiwa mazoezini,” aliandika katika ukurasa wake wa facebook.

Aishi pia alichukua fursa hiyo kuwashukuru mashabiki wa Azam FC kwa sapoti yao, ambapo aliandika kuwa: “Shukrani mashabiki kwa kunisapoti na kunipa moyo, pia kuishangilia Azam FC popote iendapo. Shukran sana kwa Azam FC kwa kunifanya niko hapa leo.”

Kipa huyo anayeibukia kwa kasi nchini hivi sasa huku pia akiaminiwa na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa, ametwaa tuzo hiyo kutokana na kiwango chake bora alichokuwa nacho hivi sasa.

Moja ya sifa yake kubwa aliyojizolea ni uwezo wake mkubwa wa kuokoa michomo ya wachezaji wa timu pinzani pamoja na kucheza kwa ustadi mikwaju ya penalti.

Katika penalti sita ilizopigiwa Azam FC msimu huu, Aishi ameokoa tatu walipoifunga Mwadui (1-0), Kagera (1-0) na sare dhidi ya Yanga (1-1), pia aliokoa mkwaju wa penalti uliopigwa na mshambuliaji wa Mwadui Kelvin Sabato na kuipeleka timu hiyo kwenye fainali ya FA Cup baada ya kuitoa Mwadui kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 120.