WACHEZAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, wamepewa mapumziko ya wiki tano baada ya kumaliza mechi ya mwisho ya msimu wa 2015/16 dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) juzi jioni.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB ambayo ni benki bora kabisa iliyosambaa kila kona nchini, ilipoteza mchezo huo wa fainali baada ya kufungwa mabao 3-1.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz  mara baada ya mchezo huo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema kuwa msimu ndio umeisha kwa timu hiyo na kilichobakia ni kujipanga kwa ajili ya kupata matokeo mazuri msimu ujao.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu tumecheza mchezo wa fainali, ingawa matokeo yalikuwa si mazuri haikuwa malengo yetu, tulipanga kushinda lakini lazima tukubali ni matokeo ya mpira,” alisema.

Kawemba alisema wachezaji watamaliza likizo hiyo Juni 30 mwaka huu na Julai Mosi wataanza maandalizi ya msimu mpya.

“Kwa hiyo tutafanya nini kwa msimu ujao, tutamuongeza nani, tutamtoa nani hayo tutazungumza baadaye lakini sasa hivi tunawaomba washabiki wetu wawe watulivu na tutaendelea kujipanga,” alisema.

Programu za vijana kuendelea

Bosi huyo aliendelea kusema kuwa kwa sasa wataendelea na programu za timu za vijana wakianza na michuano ya vijana ya Afrika Mashariki inayojulikana kama ‘Azam Youth Cup’ itakayoanza kutimua vumbi nchini kuanzia Juni 1 hadi 5 mwaka huu.

Michuano hiyo itashirikisha timu nne, Azam Academy na Future Stars Academy ya Arusha zote kutoka Tanzania pamoja na timu mbili za nje ya nchi, Football for Good Academy (Uganda) na Ligi Ndogo Academy (Kenya).

“Tutaendelea na programu za timu za vijana kwa mwezi mzima huu hadi Julai itakaporejea timu kubwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya michuano ya Kombe la Kagame,” alisema.