KOCHA Mkuu wa muda wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Dennis Kitambi, amesema kuwa udhaifu walioufanya pembeni ya uwanja ndio umepelekea kupoteza fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Yanga.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB iliweza kupoteza fainali hiyo jana jioni kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Yanga, bao la matajiri hao wa Azam Complex likifungwa na Didier Kavumbagu huku Amissi Tambwe akifunga mawili kwa upande wa Yanga na Deus Kaseka akitupia la tatu.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo Kitambi alisema Yanga wamefanikiwa kutumia vema mashambulizi yao pembeni ya uwanja na kupata mabao mawili kupitia eneo hilo.

“Kwa hiyo kutokuwa makini kuzuia mashambulizi yao pembeni ya uwanja hiyo ndio ilikuwa udhaifu, wakati wa mapumziko tulijitahidi kusema lazima tutumie njia yoyote ile ya wao kutushambulia kupitia pembeni ya uwanja, hasa hasa krosi ambazo kipindi cha kwanza zilikuwa zikitupa matatizo.

“Lakini napenda kuwapongeza wachezaji wangu walifanikiwa kupambana vizuri hata Yanga walipotangulia kutufunga bao la kwanza dakika ya tisa hata kipindi cha pili tulipofungwa bao la pili bado waliweza kujibu mashambulizi, lakini hatukuweza kutengeneza nafasi nyingi za kutosha za kuweza kushinda mchezo,” alisema.

Kitambi alichukua nafasi hiyo kusema kuwa hakuna wa kualaumiwa baada ya Azam FC kupoteza fainali hiyo kwani wameshindwa kwa pamoja kama timu na kudai kuwa kwa sasa wanatakiwa kujipanga zaidi kwa ajili ya msimu ujao.

Kocha huyo wa zamani wa Ndanda jana alisaidiana majukumu ya benchi la ufundi pamoja na Kocha Msaidizi wa Vijana wa timu hiyo, Idd Cheche, ikiwa ni mechi yao ya pili kusimamia benchi hilo baada ya ile ya kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mgambo JKT iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.

Wawili hao wameshika majukumu hayo baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Azam FC Stewart Hall kuachia ngazi akitaka kwenda kupata changamoto nyingine ya ufundishaji nje ya Tanzania.

Tayari uongozi wa Azam FC umeshaziba nafasi yake kwa kuingia mkataba na makocha kutoka nchini Hispania, Zeben Hernandez (Kocha Mkuu), Jonas Garcia (Kocha wa Viungo), huku wengine wakitarajia kuongezeka Julai mwaka huu katika eneo la Kocha wa Makipa, Kocha Msaidizi atakayesaidiana na Kitambi pamoja Daktari wa timu.