KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imezidi kujiendesha kisasa zaidi baada ya leo kuandika historia mpya ya ufunguzi wa duka lake la kuuza vifaa vyake vya michezo.

Duka hilo lililopewa jina la ‘Azam Sports Shop’ limefunguliwa eneo la Mtaa wa Swahili na Mkunguni, Kariakoo, Dar es Salaam, ambalo litakuwa ni maalumu kwa ajili ya Watanzania kununua vifaa vya Azam FC vyenye nembo ya timu hiyo zikiwemo jezi.

Baadhi ya vifaa vingine vinavyopatikana dukani hapo ni skafu, mipira, raba, mabeki ya mgongoni nay a kusukuma chini, taulo, fulana, kofia, soksi na bendera za timu hiyo.

Akizungumza wakati akizindua duka hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema hiyo ilikuwa ni ndoto yao kubwa ya muda mrefu, yote hiyo ni kutaka kuipeleka timu hiyo katika anga nyingine kabisa huku akimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufanikisha hilo.

“Tunashukuru kwa kupata duka la vifaa vya michezo litakalokuwa na bidhaa zote za Azam FC, kama mnavyoona mipira hiyo ni Azam, fulana ni Azam, kofia, viatu ni Azam, hii ni kutoa nafasi kwa washabiki wetu, kupata vifaa vya klabu yao kwa urahisi na tumefanya hivi tukiwa tumejibu maswali yao ya kila siku kuhusu upatikanaji wa vifaa hivyo.

“Pia hatukuangalia washabiki wetu tu, pia tumeziangalia familia zao kuwa wana watoto, ambao watapata mabegi ya kwenda shule, kalamu za kuandikia zenye nembo ya Azam kwa hiyo na wao wanakuwa ni sehemu ya Azam tokea wakiwa wadogo, hiyo yote ni kuona ya kwamba mzazi akiamua kuwa nyumba yake ibadilike na iwe Azam basi kila kitu kitakuwa ni Azam FC,” alisema

Kawemba alisema kuwa wanafanya mikakati kama hiyo ili kusaidia kuinua idadi ya mashabiki wa Azam FC na lengo lao ni kuona watu wakienda mazoezi wanavaa jezi za timu hiyo na hata wakienda kushangilia uwanjani basi wawe wametinga uzi wa Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati.

“Kwa hiyo tunawaomba Watanzania wote, hatuangalii ni mshabiki wa timu gani, wakaribie katika duka letu Mtaa wa Mkunguni na Swahili Kariakoo waje waone vifaa vyetu ambavyo ni halisi na sio feki na bei yake inawezekana kabisa, hatuweki kitu chenye bei kubwa, kwa hiyo tukianza na mchezo wa kesho dhidi Yanga Uwanja wa Taifa, tunataka kuona mashabiki wetu wawe wamevaa kwani kila aina ya jezi inapatikana hapa kwa watoto pia na hata wanawake,” alisema.

Alitoa wito kwa mashabiki wa timu hiyo kutumia jezi halisi za klabu na sio feki huku akisema kuwa duka hilo linafunguliwa kuanzia saa 2.30 asubuhi mpaka saa 12.30 jioni.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB kufungua duka hilo inaifanya kuingia kwenye anga za baadhi ya timu kubwa za hapa Afrika  na nyingine duniani kama vile Real Madrid, Manchester United, Barcelona, Chelsea, Arsenal, ambazo zimekuwa zikiingiza fedha nyingi kupitia mauzo ya vifaa vyao vya michezo zikiwemo jezi.