WINGA machachari wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid Mussa, amesema kuwa hivi sasa yupo fiti kukabiliana na changamoto ya soka la Hispania endapo atajiunga na Club Deportivo Tenerife msimu ujao.

Farid aliyerejea nchini jana akitokea katika timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Hispania ‘Segunda Division’, amefuzu majaribio kujiunga na timu hiyo na kinachosubiriwa hivi sasa ni kumalizika kwa mazungumzo baina ya viongozi wa Azam FC na timu hiyo iliyoonyesha nia kubwa ya kumsajili winga huyo baada ya kuridhishwa naye kwa kipindi cha mwezi mmoja alichotumia kwa majaribio hayo.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Farid alisema kuwa amekutana na changamoto nyingi sana alipokuwa kwenye majaribio ndani ya kikosi hicho hadi kufuzu, lakini hivi sasa ameshazizoea na yupo tayari kwa mapambano endapo atajiunga nayo kwa msimu ujao.

“Kwanza kule nimekutana na hali ya hewa na mandhari tofauti na hapa, pia vyakula navyo ni tofauti sana hivyo ilinichukua muda kuzoea mambo yote hayo, hata mfumo wa uchezaji na mazoezi ya wenzetu ni tofauti sana, mwanzo ilinipa shida sana lakini hivi sasa nimezoea na kuona ni kawaida sana.

“Hata wenyewe walinishangaa sana kwa namna nilivyozoea haraka na nilivyokuwa nacheza, naweza kusema nipo fiti hivi sasa kupambana na changamoto zote kule,” alisema.

Winga huyo, 20, mwenye kasi kubwa uwanjani na msumbufu kwa wachezaji wa timu pinzani kwa chenga zake za maudhi, pia alichukua fursa hiyo kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kujaalia mafanikio kwenye safari yake hiyo.

“Najisikia vizuri sana kufuzu majaribio na namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa hatua niliyofika, watu wa kule Hispania wameonyesha kunikubali sana na najivunia kwa hilo kiukweli nimefurahishwa na hilo sana, kwa hiyo mimi ni juhudi tu nitakazoziongeza kwenye mazoezi kwani malengo ninayoyataka mimi na sehemu ninayotaka nifike bado sana na ndio maana napambana sana niwezavyo,” alimalizia.

Farid aliyekuzwa kwenye kituo cha kulelea vipaji cha Azam FC ‘Azam FC Academy’, hadi anapata nafasi hiyo ya kwenda Hispania kwa kiasi fulani imechangiwa na kiwango chake bora msimu huu baada ya kuchezeshwa mara kwa mara katika kikosi cha timu kubwa.

Moja ya bao lake litakalokumbukwa msimu huu ni lile alilofunga dakika za mwisho kwenye mchezo mgumu wa robo fainali ya Kombe la Kagame Julai mwaka jana dhidi ya mabingwa wa Uganda KCCA, ambalo liliifanya Azam FC kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa bao 1-0.

Hatimaye Azam FC inayoshaminiwa na Benki ya NMB, ikatinga tena fainali kwa kuitupa nje Yanga na kuchukua ubingwa huo kwa mara ya kwanza kihistoria bila kuruhusu bao wala kufungwa mchezo wowote, ikiwachapa mabingwa wa Kenya Gor Mahia mabao 2-0.