KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, sasa itakipiga na Yanga kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) katika tarehe ya awali Mei 25 mwaka huu ndani ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kubadilishwa tena kwa fainali hiyo kutoka Juni 11 iliyopangwa hivi karibuni, kumefikiwa jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kikubwa wakidai imeachwa tarehe ya awali ili kuenenda na kanuni ya tarehe ya mashindano kufuatia mwisho wa msimu kuwa ni Mei 31, mwaka huu.

Wakati TFF inabadilisha tarehe ya awali kutoka Mei 25 hadi Juni 11, ilidai kuwa inataka kuzipa muda wa kuajindaa timu mara baada ya mechi za mwisho za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) Mei 22 mwaka huu.

Kadhalika tarehe ya awali ilipangwa kutokana na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kuwa na ratiba ya kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa ulioko kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’ Mei 29, mwaka huu jijini Nairobi Kenya.

Lakini uongozi wa Azam FC ukafanya jitihada za kuiomba TFF kurudisha tarehe ya awali kutokana na tarehe hiyo mpya (Juni 11, 2016) kutoendana na kalenda ya matukio ya msimu huu ambao unamalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Tayari Azam FC inayodhaminiwa na Benki na NMB, imeshajitwalia nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani hata kama haitatwaa taji la FA Cup na hii ni kutokana na Yanga itakayocheza nayo kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.

Lakini moja ya malengo makubwa iliyojiwekea Azam FC mara baada ya kuukosa ubingwa wa ligi ni kuhakikisha inatwaa taji hilo, ambalo litaifanya kumaliza msimu ikiwa na rekodi nzuri ya kutwaa mataji mawili jingine likiwa ni la ubingwa wa michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), walilotwaa bila kufungwa mchezo wala kuruhusu bao ndani ya dakika 90.

Huku pia ikifukuzia rekodi nyingine ya kumaliza kwenye nafasi mbili za juu ndani ya ligi kwa msimu wa tano mfululizo, licha ya kuwa timu changa iliyoanzishwa mwaka 2007 ikacheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu msimu wa 2008/09 na ikajiandikia rekodi ya kutwaa taji la kwanza wa ligi 2013/14 kwa rekodi ya kutofungwa mchezo wowote. 

Azam FC, Yanga zilivyotinga fainali

Azam FC ilitinga fainali baada ya kuichapa Mwadui ya Shinyanga kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia dakika 120 kuisha kwa sare ya mabao 2-2, mchezo wa nusu fainali uliofanyika Uwanja wa Mwadui, Shinyanga.

Katika hatua za awali Azam FC ilizitoa African Lyon (4-0), Panone (2-1), zote ikicheza ugenini na ikatinga nusu fainali kwa kuwalamba maafande wa Tanzania Prisons mabao 3-1 nyumbani ndani ya Uwanja wa Azam Complex.

Yanga yenyewe ilisubiria kupita kwa uamuzi wa mezani kufuatia mchezo wao wa nusu fainali dhidi ya Coastal Union kuvunjika wakati wakiongoza wa mabao 2-1 kufautia mashabiki wa Wagosi wa Kaya hao kuanzisha vurugu kwa kutokukubalina na uamuzi wa waamuzi.

Wanajangwani hao awali walianza kuwapiga Friends Rangers (3-0), JKT Mlale (2-1), Ndanda (2-1), zote ikicheza nyumbani katika Uwanja wa Taifa kabla ya kucheza ugenini kwa mara ya kwanza katika nusu fainali dhidi Coastal Union.