KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imedhidhirisha ya kuwa imepania kumaliza katika nafasi ya pili msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa African Sports mabao 2-1.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 63 katika nafasi ya pili ya ligi na kuiacha Simba kwa pointi moja iliyonafasi ya tatu huku Yanga ikiwa tayari imetetea taji lao baada ya kufikisha jumla ya pointi 72.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB iliuanza vema mchezo huo na ikaweza kuandika bao la uongozi katika dakika 10 ya mchezo lililofungwa kwa kichwa na mshambuliaji Allan Wanga aliyemalizia pasi ya kichwa ya nahodha wa mchezo wa leo Himid Mao ‘Ninja’ aliyeunganisha vema kona iliyochongwa na Khamis Mcha ‘Vialli’.

Hilo ni bao la pili la Wanga ndani ya ligi msimu huu na la tatu katika mashindano yote, jingine akitupia wakati Azam FC ilipoichapa Panone mabao 2-1 kwenye hatua ya 16 ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Dakika moja baadaye African Sports iliweza kusawazisha bao hilo kupitia kwa Omary Ibrahim aliyetumia vema uzembe wa mabeki wa Azam FC walioshindwa kuokoa vizuri mpira uliokuwa ukizagaa langoni mwao.

Bao hilo liliwapa nguvu African Sports, ambao walionekana kuja na nguvu mpya na kulisakama mara kwa mara lango la Azam FC, ambao walipoteza umiliki wa mipira katikati ya uwanja.

Lakini hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu hizo zilitoka uwanjani zikiwa nguvu sawa kwa mabao hayo, Azam FC iliimarisha eneo lake la ushambuliaji kipindi cha pili baada ya kumpumzisha Khamis Mcha na kuingia kinda Shaaban Idd.

Mabadiliko hayo yaliiongezea kasi eneo la ushambuliaji la Azam FC na hatimaye katika dakika ya 74 iliweza kupata bao la pili kupitia kwa beki mkongwe, Erasto Nyoni, aliyepiga shuti kali ndani ya eneo la hatari kufuatia kuufumania mpira uliokuwa ukizagaa langoni mwa Sports kufuatia kona iliyochongwa na Ramadhan Singano ‘Messi’.

Licha ya Sports kuongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Azam FC ili kusawazisha bao hilo, walijikuta wakimaliza dakika 90 kwa kukubali kipigo hicho, ambacho kiliwanyong’onyesha wachezaji wake.

Katika hatua nyingine, makocha wapya watarajiwa wa Azam FC kutoka nchini Hispania Kocha Mkuu Zeben Hernandez na Kocha wa Viungo Jonas Garcia, walipata fursa ya kushuhudia mchezo huo na kujionea aina ya wachezaji watakaokwenda kufanya nao kazi msimu ujao baada ya kocha wa sasa, Stewart Hall, kutangaza kuachia ngazi mwishoni mwa msimu huu. 

Matokeo hayo ya mechi hiyo iliyofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga yamezidi kuiweka kwenye wakati mgumu African Sports katika vita yake ya kuepuka kushuka daraja msimu huu.

Hiyo inatokana na ushindi wa Kagera Sugar (2-1) dhidi ya Stand United jioni ya leo na hivyo hivi sasa itakuwa ikiziombea mabaya Kagera na Mgambo JKT ziteleze kwenye mechi zao za mwisho na yenyewe ishinde ili iweze kusalia Ligi Kuu.

Mpaka sasa ligi ikielekea kumalizika wikiendi ijayo Mei 21, timu nne za Mgambo JKT (27), African Sports (26) zote za Tanga, Kagera Sugar (28) na JKT Ruvu (29), bado zipo kwenye hatari ya kushuka daraja, ambapo mbili kati ya hizo zitaungana na Coastal Union (Tanga) ambayo ndio timu pekee iliyoshuka daraja hadi sasa.

Ushindi wowote wa Azam FC kwenye mchezo wake wa mwisho dhidi ya Mgambo JKT utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex utakuwa umewashusha rasmi daraja maafande hao.

Vikosi vilikuwa hivi:

Azam FC: Aishi Manula, Abdallah Kheri, David Mwantika, Erasto Nyoni, Wazir Salum/Gadiel Michael dk 84, Himid Mao, Michael Bolou/Mudathir Yahya dk 75, Salum Abubakar, Khamis Mcha/Shaaban Idd dk 46, Allan Wanga, Ramadhan Singano

African Sports: Kabali Faraji, James Mendi/Ally Ramadhan dk 61, Mwaita Gereza, Issa Shaaban, Juma Shemvuni, Rahim Abdallah, Mussa Chambega, Hassan Materema, Omar Ibrahim, Rajab Isihaka/Mohamed Mtindi dk 85, Ayoub Mrisho