TIMU ya vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ‘Azam Academy’,le imezidi kufanya kweli baada ya kuichapa Makumbusho FC mabao 5-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Ushindi huo wa Azam Academy unaifanya kulipa kisasi cha kufungwa bao 1-0 na timu hiyo katika mchezo wao wa kwanza uliofanyika mwezi uliopita.

Azam FC ilitakata zaidi kipindi cha kwanza ikicheza soka la kasi jambo ambalo liliwafanya kumaliza kipindi hicho ikiwa na uongozi wa mabao matatu.

Alikuwa ni Mohamed Sadalah aliyeanza kuipatia bao la uongozi timu hiyo kabla ya Rajabu Odasi na Optatus Lupekenya kuongeza mengine na mpira huo kwenda mapumziko.

Kipindi cha pili Makumbusho walionekana kubadilika na kucheza vema hali ambayo iliwafanya kuweka kufunga mabao mawili ya kufuatia machozi.

Lakini Azam Academy iliyochini ya kocha raia wa Uingereza, Tom Legg na Msaidizi wake, Idd Cheche, ilijihakikishia ushindi huo mnono kwa kuongeza mabao mengine mawili kupitia kwa Sadalah na Optatus.

Wawa autumia kujifua

Katika mchezo huo ilishuhudiwa beki wa timu kubwa ya Azam FC, Pascal Wawa, akiingia dakika 10 za mwisho kujiweka sawa kufuatia kuanza kupata nafuu ya majeraha yake kwenye maungio nyuma ya goti.

Wawa alipata majeraha hayo wakati Azam FC ikiichapa Esperance ya Tunisia mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Beki huyo kikisi raia wa Ivory Coast alionekana bado kutokuwa fiti kutokana na kucheza kwa uoga huku akishindwa kugombani mipira dhidi ya wachezaji wa Makumbusho FC na kwa mujibu wa jopo la kitabibu la Azam FC inaelezwa kuwa anahitaji muda zaidi wa kurejea katika hali yake ya kawaida na kuanza kuonekana dimbani.