NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, ameingia kwenye orodha ya wachezaji majeruhi wa timu hiyo baada ya misuli yake ya mguu kukaza.

Tokea jana mshambuliaji huyo amekuwa akipewa programu maalum ya kufanya mazoezi ‘gym’ ili kuirejesha vizuri sawa misuli yake, hali ambayo inamfanya kuukosa mchezo ujao dhidi ya African Sports utakaofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumapili ijayo (Mei 15, 2016).

Mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa nyota huyo hana nafasi ya kucheza mchezo huo kutokana na majeraha hayo aliyopata huku pia akiendelea kuwakosa mabeki Shomari Kapombe, Pascal Wawa, kiungo Frank Domayo.

Alisema wachezaji wengine ambao wana hatihati ya kuwemo kwenye mchezo huo ni mshambuliaji Khamis Mcha ‘Vialli’ (matatizo ya nyonga) na kiungo Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ mwenye majeraha ya nyama za paja, amedai kuwa nyota hao wataangaliwa maendeleo yao ya afya kesho kabla ya kujulikana kama wapo fiti au la.

“Tutacheza mchezo wetu wa mwisho ugenini msimu huu dhidi ya African Sports, tunataka kushinda mchezo huo, najua utakuwa mchezo mgumu kwani wenzetu wanapambana kutoshuka daraja na pia ubovu wa uwanja tutakaochezea.

“Lakini tunajua namna ya kupambana nao, mfumo tutatumia ule ule wa 4-3-3, ukiangalia mpaka sasa mchezo pekee tuliopoteza ugenini ni ule dhidi ya Coastal Union (1-0) ni rekodi nzuri na ndio maana tunataka kushinda na huo, pia ili tumalize nafasi ya pili tukiwa na pointi nzuri,” alisema Hall.

Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kesho mara baada ya mazoezi ya asubuhi kuelekea mkoani Tanga, ambapo Jumamosi asubuhi kitafanya mazoezi ndani ya Uwanja wa Mkwakwani kabla ya kuvaana na timu hiyo.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ambayo ni benki bora iliyosambaa kote kabisa nchini Tanzania, imejikusanyia jumla ya pointi 60 na inahitaji ushindi katika mechi zake mbili zilizobakia ili kuiondoa Simba (59) kwenye mbio za kuwania nafasi ya pili huku Yanga ikiwa tayari imeshaetea ubingwa wa ligi hiyo.

African Sports yenye pointi 26 inahitaji ushindi katika mechi zake mbili zilizobakia ili kujihakikishia nafasi ya kusalia kwenye ligi na kuwapoteza Kagera Sugar (25), Mgambo JKT (24), ambao wapo chini yake wakihangaika kujinasua huku Coastal Union ikiwa tayari imeshashuka daraja.

Mtanange wa kwanza baina ya timu hizo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, uliisha kwa sare ya bao 1-1, Azam FC ilianza kufunga bao la kwanza kupitia kwa kiungo Frank Domayo ‘Chumvi’, aliyepiga shuti kali kabla ya Hamad Mbumba kuisawazishia Sports.