WADHAMINI wakuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Benki ya NMB leo asubuhi wametembelea makao makuu ya klabu hiyo Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Huu ni mwaka wa pili tokea benki hiyo bora iliyosambaa kila kona nchini, ianze kuwadhamini mabingwa hao wa michuamo ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup).

Mara baada ya kuwasili ndani ya viunga hivyo, msafara huo wa wafanyakazi wa NMB ulipata fursa ya kusalimiana na wachezaji pamoja na benchi la ufundi la Azam FC pamoja na kupiga nao picha za ukumbusho.

Pia lilifanyika zoezi la wachezaji kutia saini zao kwenye mpira maalumu uliondaliwa na wafanyakazi wa Benki ya NMB ikiwa ni kama ukumbusho, huku wengine wakipata fursa ya kuzungumza pamoja na nyota wa kikosi hicho kilichotinga fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) itakayofanyika Juni 11 mwaka huu.

Wajionea mazingira ya Azam FC

Katika hatua nyingine wafanyakazi hao wa Benki ya NMB walipata fursa ya kutembelea mandhari ya viunga hivyo wakianzia kwenye ‘gym’ ya kisasa pamoja na bwawa la kuogelea wachezaji.

Vilevile walitembelea chumba maalumu cha kuwafanyia matibabu wachezaji pamoja na eneo la kuhifadhia makombe iliyoshinda Azam FC tokea kuanzishwa rasmi mwaka 2007 na kupanda Ligi Kuu mwaka 2008.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake wa Benki ya NMB, kiongozi wa msafara huo ambaye ni Meneja Uhabarishaji Mitandao ya Jamii, Bi. Joyce Nsekela, alisema kuwa wamefurahishwa sana kupata fursa hiyo ya kutembelea timu hiyo.

“Tunashukuru sana kwa kutupa nafasi hii, sisi kama wadhamini wenu tumefurahishwa sana na ziara yetu hapa, tumejionea kila kitu kinachofanyika hapa na kukutana na wachezaji ambao hatujawahi kuwaona, ni jambo zuri, nadhani tutapata muda mrefu zaidi siku nyingine wa kuja hapa na kufurahia zaidi,” alisema.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Benki ya NMB ilizindua kampeni maalumu kwa mashabiki wa Azam FC inayojulikana kwa jina la #AzamFCShabikiWaKweli, ambayo itawapa fursa mashabiki 10 washindi kukutana na timu hiyo hivi karibuni na kujishindia zawadi kadhaa ikiwemo mipira na jezi mpya za Azam FC.

Uongozi wa Azam FC tunazidi kufarijika na udhamini huu wa Benki ya NMB kwani umekuwa chachu ya mafanikio yetu msimu huu mpaka sasa tukiwa tumetwaa ubingwa wa Kombe la Kagame na tukiwa kwenye harakati za kuwania taji la Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) tukiwa tumeingia fainali ambayo tutacheza na Yanga Juni 11 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,