UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika na Kati Azam FC, tayari umekata rufaa kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) tokea Jumamosi iliyopita kupinga uamuzi wa kukatwa pointi tatu kwa kumchezesha mchezaji Erasto Nyoni.

Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara (TPLB) ilitangaza uamuzi huo Mei 5 mwaka huu wakidai beki huyo alichezeshwa kimakosa na Azam FC  katika mchezo dhidi ya Mbeya City (Februari 20, 2016) uliofanyika Uwanja wa Sokoine wakidai kuwa alikuwa na kadi tatu za njano.

TPLB ilidai kuwa Nyoni alikusanya kadi hizo katika mchezo wa ngao wa jamii dhidi ya Yanga, mchezo wa kwanza wa ligi waliocheza na Tanzania Prisons Azam Complex na ule wa Coastal Union uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Februari 14 mwaka huu, hivyo alitakiwa kutocheza mchezo uliofuata dhidi ya Mbeya City.

Bodi hiyo ilisema kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 37(4) ya Ligi Kuu Toleo la 2015 inayoelekeza kuwa mchezaji atakayeonywa kwa kadi ya njano katika michezo mitatu hataruhusiwa kucheza mchezo unaofuata wa timu yake. Hivyo kwenda kinyume na kanuni husika.

“Pia kwa kuzingatia Kanuni ya 14(37) ya Ligi Kuu Toleo la 2015, timu ya Mbeya City imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu,” ilieleza taarifa hiyo.

Lakini kwa mujibu wa mapitio ya mechi yaliyofanywa na Azam FC imebainika ya kuwa Nyoni alikusanya kadi ya tatu ya njano kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons uliofanyika Februari 24, 2016 ndani ya Uwanja wa Sokoine, mechi mbili nyingine za nyuma alizokusanya kadi ni dhidi ya Yanga katika Ngao ya Hisani na ule wa Coastal Union (Tanga).

Hivyo baada ya kukusanya kadi ya tatu ya njano dhidi ya maafande hao, Nyoni aliukosa mchezo uliofuata dhidi ya Yanga  uliofanyika Uwanja wa Taifa Machi 5 mwaka huu na kuisha kwa matokeo ya sare mabao 2-2.

Taarifa za awali zilisema kuwa beki huyo alianza kukusanya kadi ya pili ya njano kwenye mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons uliofanyika Septemba 12 mwaka jana, lakini kwa mujibu wa mapitio hayo imebainika ya kuwa wachezaji pekee waliokusanya kadi kwa upande wa Azam FC siku hiyo ni beki Pascal Wawa na winga Farid Mussa.