SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefanya marekebisho ya tarehe ya mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), kutoka Mei 25 tarehe ya awali na sasa itafanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Juni 11 mwaka huu.

Fainali hiyo itazikutanisha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC watakaikipiga na Yanga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa jana na TFF imeeleza kuwa Rais wa Shirikisho hilo, Jamal Malinzi, amesema tarehe hiyo ni muafaka kulingana na kalenda ya shughuli mbalimbali za soka nchini.

“Ratiba na kalenda hiyo inaonyesha kuwa Ligi Kuu ya Vodacom inatarajiwa kufikia kikomo Mei 21, 2016 kabla ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kuitwa kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’ unaotarajiwa kufanyika Mei 29, mwaka huu,” ilisema taarifa hiyo.

Taifa Stars itacheza mechi hiyo ikiwa ni maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Misri unaotarajiwa kufanyika Juni 4, 2016 Dar es Salaam kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Gabon mwakani.

Tayari TFF imefafanua kuwa iwapo Bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa msimu huu inayoendelea atashinda pia taji la FA Cup, ndiye atayeiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika mwakani.

Kwa msingi huo, timu itakayopoteza katika fainali ya michuano ya FA Cup inayodhaminiwa na Kituo cha Televisheni cha Azam, ndiyo itakayowakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB imetinga fainali ya michuano hiyo baada ya kuwatoa mashindanoni Mwadui ya Shinyanga kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 120 za mchezo huo.

Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, ameshaweka wazi kuwa anautaka ubingwa wa michuano hiyo ili aweze kuiongezea rekodi timu hiyo ya kutwaa mataji mawili msimu huu.

Taji la kwanza ni lile la Kombe la Kagame walilolitwaa Agosti mwaka jana Dar es Salaam, baada ta kuichapa Gor Mahia ya Kenya kwenye fainali kwa jumla ya mabao 2-0 yaliyofungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na Kipre Tchetche.