KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jioni ya leo itashuka kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga kuvaana na wenyeji wao Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, itaingia dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare mechi mbili zilizopita dhidi ya Simba (0-0) na JKT Ruvu (2-2), matokeo ambayo yamefifisha mbio zao za ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Walikuwa ni mabingwa hao wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) walioibuka na ushindi kwenye mchezo wa raundi ya kwanza kwa bao 1-0 lililofungwa na beki kisiki Shomari Kapombe akipokea pasi safi ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’.

Lakini mchezo wa safari unakuja kivingine na vita kuu mbili baina ya timu hizo, Azam FC ikitaka kushinda mechi zake tatu zilizobakia ili kuhakikisha inashika nafasi ya pili huku Kagera Sugar wenyewe wakipagana kutoshuka daraja.

Azam FC inahitaji kukusanya pointi tisa na kufikisha pointi 66 kwa kushinda mechi hizo tatu dhidi ya Kagera Sugar leo, African Sports Mei 15 na ya mwisho Mei 21, mwaka huu watakayokipiga na Mgambo JKT ndani ya dimba la Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ili kupigania nafasi ya pili wakizidiwa pointi moja tu na Simba iliyofikisha 58 na wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

Vita ya ubingwa tayari Yanga inaelekea kuishinda Mei 10 mwaka huu watakpocheza na Mbeya City ndani ya Uwanja wa Sokoine kwani wanahitaji pointi tatu tu na kufikisha junla ya pinti 71, ambazo hazitaweza kufikiwa na Simba iliyonafasi ya pili kwani hata wakishinda zote nne walizobakiza watafikisha 70 tu.     

Kagera Sugar iliyo katika nafasi tatu za chini kwenye janga la kushuka daraja ikiwa nafasi ya 14 imejikusanyia pointi 25 na/ inahitaji pointi nane tu ndani ya mechi zake tatu zilizobakia ili kujihakikishia nafasi ya kubakia Ligi Kuu kwani itatimiza 33, ambazo haziwezi kufikiwa na African Sports aliyejuu yake kwa pointi 26 hata kama atashinda mechi zake mbili zilizobakia.

Tayari Coastal Union imeshakuwa timu ya kwanza kushuka daraja msimu huu mara baada ya kufungwa na Stand United mabao 2-1 jana jioni kwenye Uwanja wa Kambarage, nyingine ambayo ipo kwenye hatari ya kushuka daraja ni African Sports inayohitajika kushinda mechi zake mbili zijazo pamoja na JKT Ruvu inayohitaji pointi nne tu ili ijiondoe kwenye janga hilo.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwakosa baadhi ya nyota wake kama mabeki Pascal Wawa, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Wazir Salum, kiungo Frank Domayo, ambao wote ni wagonjwa huku kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, akikosekana kutokana na kukusanya kadi tatu za njano.

Mwingine ni winga Farid Mussa, ambaye amekwenda kwenye majaribio nchini Hispania.  

Mpaka sasa Azam FC imecheza jumla ya mechi 27 ikiwa imeshinda 16, sare tisa na kufungwa mara mbili, moja ilipoteza kwa kupokonywa pointi tatu baada ya kuchezeshwa beki Erasto Nyoni, aliyekuwa na kadi tatu za njane kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City uliofanyika Februari 20, mwaka huu mjini Mbeya na matajiri hao kushinda 3-0.

Kagera Sugar yenyewe katika mechi 27 ilizocheza, mpaka sasa imeshinda sita tu na kupoteza 14.