TIMU ya Azam Veteran usiku wa kuamkia leo imeaga michuano ya Ligi ya JMK Floodlight baada ya kufungwa na JMK-Romario Sports kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia saye ya 2-2 ndani ya muda wa kawaida wa mchezo huo wa hatua ya robo fainali.

Azam Veteran hadi inatinga hatua hiyo iliweza kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi baada ya kuongoza Kundi A, lakini bahati haikuwa yao katika mchezo huo wa robo fainali kutokana na kukosa mabao mengi ya wazi hasa kipindi cha pili.

Mabao ya Azam Veteran yalifungwa na Amiri Rashid ‘Kikwa’ aliyefunga bao la kwanza huku nahodha wa kikosi hicho mshambuliaji hatari, Abdulkarim Amin ‘Popat’, akipigilia msumari wa pili, yote yakiwa ni ya kusawazisha kufuatia JMK kutangulia kupata mabao.

Azam Veteran ilicheza vizuri sana kipindi cha pili kwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao kupitia kwa wakali wake Philip Alando, Salim Aziz ‘Mahrez’ na Popat waliokuwa wakiisumbua sana safu ya ulinzi ya JMK, lakini mashuti mengi waliyokuwa wakipiga yalishindwa kujaa wavuni.

Hivyo hadi mpira huo uliochezeshwa na mwamuzi mkongwe Othman Kazi, unamalizika matokeo yalibakia kuwa sare hiyo na ndipo JMK waliweza kuibuka kidedea kwa ushindi wa penalti 4-3.

Baadhi ya wachezaji wengine wanaounda kikosi cha Azam Veteran ni Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Idrissa Nassor, Meneja Luckson Kakolaki na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar, timu hiyo ikifundishwa na Kocha Msaidizi wa Azam FC Academy, Idd Cheche.

Michuano hiyo inayofanyika katika kituo cha michezo cha JMK Youth Park, kilichopo Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, ni maalumu kwa ajili ya timu za maveterani wenye umri kuanzia miaka 30 huku wachezaji watatu tu wakitakiwa kusajiliwa na kila timu kwa wale waliochini ya umri huo.