TIMU ya vijana ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jana iliwacharaza vijana wenzao wa Simba mabao 2-0 katika mchezo wa utangulizi kabla ya mechi ya wakubwa.

Imekuwa ni sheria kila zinapochezwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) basi ni lazima zitangulie mechi za timu za vijana.

Kikosi hicho cha Azam FC Academy kinachonolewa na Kocha kutoka Uingereza, Tom Legg na Msaidizi wake Idd Cheche ambaye ni mzawa, kimekuwa na rekodi nzuri ya ushindi kila kinapocheza mechi zake za kirafiki.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake, uliamuliwa na staa wa Azam FC Academy, Shaaban Idd, aliyefunga mabao mawili yote, la pili akifunga kwa ustadi mkubwa kwa mkwaju wa moja kwa moja wa adhabu ndogo umbali wa takribani Mita 30.

Mara baada ya kufunga bao hilo, Idd alikimbia kwa furaha kubwa huku akishangilia na kwenda kuwakumbatia makocha wa timu kubwa ya Azam FC, Stewart Hall na Msaidizi Mario Marinica, ambao walikuwa wakishuhudia mchezo huo.

Idd ni mmoja ya wachezaji watatu waliopandishwa kucheza timu kubwa msimu huu, wengine wakiwa ni nahodha wa wao, kiungo Abdallan Masoud ‘Cabaye’ na beki wa kati Adolph Mtasingwa.

Hadi dakika 90 zinamalizika Azam FC Academy, iliondoka na ushindi huo mzuri na sasa keshokutwa Jumatano itavaana na timu ya vijana ya JKT Ruvu kabla ya mchezo wa timu zao kubwa.