KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jjana imetoka sare ya bila kufungana na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu zote mbili zilianza mchezo huo kwa kasi ya chini, na walikuwa ni Simba waliopata nafasi ya kwanza ya kufunga bao katika dakika ya pili baada ya Hamis Kiiza kupiga kichwa kizuri kilichotolewa kiustadi na kipa mahiri wa Azam FC Aishi Manula.

Ndani ya dakika 12 za mwanzo Azam FC ingeweza kuwa mbele kwa mabao matatu kama vichwa viwili vizuri alivyopiga nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’ vingejaa wavuni, ambavyo vilitoka sentimita chache ya lango la Simba.

Nafasi nyingine ya wazi katika dakika hizo, aliikosa mshambuliaji Khamis Mcha ‘Vialli’, akiwa na kipa wa Simba, Vincent Angban’, baada ya kuunasa mpira kufuatia uzembe wa mabeki wa wekundu hao, lakini shuti alilopiga lilimlenga kipa huyo aliyeudaka vema mpira.

Kwa dakika zote zilizobakia za kipindi cha kwanza, timu zote mbili zilionekana kushambuliana kwa zamu lakini tatizo kubwa kwa kila upande lilikuwa ni kukosekana ubunifu wa kupenya ngome ya ulinzi ya mwenzake.

Mabadiliko ya Azam FC kuwaingiza Mudathir Yahya na Ame Ally kipindi cha pili yalisaidia kuamsha na kuongeza kasi eneo la ushambuliaji, lakini tatizo liliendelea kubakia lilelile na kushindwa kutumia vema nafasi wazilizozipata kupitia kwa Mudathir na Bocco na hivyo kufanya hadi dakika 90 zinamalizika timu zote ziondoke uwanjani kwa kugawana pointi moja kila mmoja.

Sare inamaanisha nini?

Sare hiyo imeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 59 katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, Simba ikiwa imejikusanyia 58 katika nafasi ya tatu huku Yanga ikiwa kileleni kwa pointi 65.

Hivyo sare ya timu hizo imeibeba Yanga kwenye mbio za ubingwa kwani wakati mechi za ligi zikiwa zimebakia nne kwa kila timu ili imalizike, Wanajangwani hao wanahitaji pointi saba tu (yaani ushindi mara mbili na sare moja) ndani ya mechi tatu zijazo ili kutetea taji lao kwani watafikisha jumla ya pointi 72 ambazo haziwezi kufikiwa na Azam FC wala Simba.

Yanga itaupoteza ubingwa huo ikiwa watafungwa mechi mbili zijazo na kutoa sare moja, ambapo Azam FC kama yenyewe itashinda mechi zake zote itakuwa imelitwaa taji hilo kwa mara ya pili kihistoria baada ya kufanya hivyo msimu wa 2013/14 bila kufungwa mchezo hata mmoja.

Vikosi vilikuwa hivi:

Azam FC: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Aggrey Morris, David Mwantika, Jean Mugiraneza/Kipre Balou dk 76, Ramadhan Singano ‘Messi’/Mudathir Yahya dk 46, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Kipre Tchetche/Ame Ally ‘Zungu’ dk 65, John Bocco na Khamis Mcha ‘Vialli’.

Simba: Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid/Brian Majwega dk 74, Novart Lufunga, Justise Majabvi, Awadh Juma, Jonas Mkude, Hamisi Kiiza, Danny Lyanga/Hajji Ugando dk54/Mussa Mgosi dk 90 na Peter Mwalyanzi.