KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, itakuwa na kibarua kizito kupambana na Simba katika mchezo unaotarajia kuamua vita vya ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) vya timu hizo mbili, utakaofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kesho Jumapili saa 10.00 jioni.

Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 58 na Simba 57 katika nafasi ya tatu, kwa pamoja zinaifukuzia Yanga katika mbio hizo za ubingwa, ambayo ipo kileleni baada ya kufikisha jumla ya pointi 62 kabla ya mchezo wao wa jioni ya leo dhidi ya Toto Africans.

Mabingwa hao wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) imefanya maandalizi ya nguvu kukabiliana na Wekundu hao, ambao wenyewe walienda kujichimbia visiwani Zanzibar kujiandaa na mtanange huo, hivyo mchezo huo unatarajia kuwa na upinzani mkali kwa pande zote mbili.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi katika mchezo uliopita dhidi ya Majimaji ya Songea (2-0) mabao yote yakifungwa na kiungo Mudathir Yahya, huku bao pekee lililofungwa na mshambuliaji wa Toto Africans, Wazir Junior, likiizamisha Simba ndani ya Uwanja wa Taifa.

Hall asema; Azam FC ni ushindi tu

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya mwisho leo asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa ushindi kwao ni jambo muhimu kesho kama wanataka kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

“Kama mchezo huo utakuwa sare basi haitakuwa nzuri kwetu sisi na Simba katika mbio za kutwaa ubingwa, kama tunataka nafasi ya pili basi ni nzuri, lakini sisi hatutaki nafasi ya pili tunataka nafasi ya kwanza, hivyo lazima tushinde na hata wachezaji wana morali hiyo na kutambua hilo, kwani sare itampa nafasi Yanga kujihakikishia ubingwa,” alisema.

Hall alisema kuwa hawatakuwa na presha kubwa katika mchezo huo kama watakayokuwa nayo wapinzani wao, hii ni kutokana na wekundu hao kupigania nafasi ya pili na ya kwanza, hivyo presha yao kubwa itakuwa ni kutufunga sisi.

“Maandalizi yetu kwa kiasi kikubwa yameandamwa na baadhi ya wachezaji wetu kuwa majeruhi wengine wakiwa ni wagonjwa, Wazir (Salum) hataweza kucheza kutokana na mbavu yake kupata ufa, lakini wachezaji watatu walioukosa mchezo wa Majimaji watarejea kikosini, Bolou (Michael), Kipre Tchetche waliokuwa majeruhi pamoja na Bocco (John) tuliyempumzisha hivyo kikosi chetu kitakuwa imara,” alisema.

Azam FC itawakosa wachezaji wengine kama kiungo Frank Domayo, Allan Wanga, Racine Diouf, Shomari Kapombe, ambao ni wagonjwa huku Nahodha Msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, akiendelea kukosekana kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata wakati timu hiyo ikiichapa Mtibwa Sugar bao 1-0.   

Akizungumzia presha wanayokuwa nayo wachezaji wake kila wanapocheza mechi dhidi ya Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Hall alisema kuwa hiyo inatokana na waamuzi wanaochezesha mechi hizo pamoja na mashabiki wengi wa timu hizo wanaojazana ndani ya uwanja huo.

“Najua kesho uwanja utajaa kwani mashabiki wa Yanga nao watavutika na huo mchezo na watakuwa wakiombea tutoke sare kwa kuwa itakuwa imetuua sisi na Simba katika mbio za ubingwa, mechi nyingi zilizopita tulizocheza ndani ya uwanja huo viwango vya waamuzi vimekuwa chini sana, hivyo kesho natarajia ubora wa waamuzi na haki,” alisema.

Vita ya Mwingereza vs Mganda

Pambano la kwanza lililpigwa Desemba 12 mwaka jana, ilikuwa ni vita vya Waingereza baina ya Hall na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba kutoka Uingereza, Dylan Kerr, ambaye ameshafutwa kazi mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu.

Azam FC haijabadilisha hata sura moja kwenye benchi lake la ufundi na safari hii Simba itakuwa chini ya Mganda, Jackson Mayanja, ambaye atakuwa jukwaani kushuhudia mchezo huo kutokana na kutolewa katika benchi la ufundi na mwamuzi wakati Simba ilipochapwa na Toto Africans.

Licha ya kupoteza mchezo dhidi ya Toto Africans, Simba kabla ya kuingia kwenye mechi hiyo ilitoka kupoteza mchezo mwingine wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kwa kufungwa na Coastal Union mabao 2-1.

Rekodi zao VPL (Head to Head)

Mpaka sasa timu hizo zikiwa zimeshacheza mechi 25 kila mmoja msimu huu, Azam FC imeshinda jumla ya mechi 17 kati ya hizo, ikitoa sare saba na kufungwa mmoja huku Simba ikishinda 18, sare tatu na kupigwa mara nne, jambo la kuvutia zote zimefunga jumla ya mabao 43 kila mmoja, lakini Azam FC imeruhusu mabao 16 na Wekundu hao 14.

Hadi timu hizo zinakutana tena kesho, mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliisha kwa sare ya mabao 2-2, nahodha John Bocco ‘Adebayor’ akifunga mabao pekee kwa upande wa Azam FC na Ibrahim Ajibu akiifungia Simba mabao hayo.  

Kihistoria timu hizo zimekutana mara 15 kwenye ligi, tokea Azam FC ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008/2009, Azam imeshinda mara nne, Simba mara saba na mechi nne zimeisha kwa sare.