KIUNGO wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Mudathir Yahya, amesema kuwa mabao yake mawili aliyofunga jana dhidi ya Majimaji ya Songea yamechangiwa na kujituma mchezoni.

Mudathir jana aliiwezesha Azam FC kutinga hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kufikisha pointi 58 baada ya kufunga mabao pekee yaliyoipata timu yake ushindi wa 2-0 dhidi ya Wanalizombe hao.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Mudathir alisema kutokana na kutopata muda mwingi wa kucheza msimu huu, alipanga kuonyesha kitu cha utofauti jambo ambalo amefanikiwa.

“Najisikia furaha kufunga, nilijiuliza kwanini kocha anipi nafasi, hivyo nikatumia juhudi zangu zote kufanya kitu cha utofauti jana ili nizidi kupewa nafasi zaidi ya kucheza katika mechi zijazo,” alisema.

Kiungo huyo fundi anayeichezea timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ na kuwahi kuitwa katika kikosi cha Tanzania ‘Taifa Stars’, aliongeza kuwa: “Hali ya kujituma iliongezeka zaidi kipindi cha pili hasa baada ya walimu kutuambia tuongeze kasi, nilifanikiwa kuongeza kasi na kufunga mabao hayo, naamini nikipewa nafasi zaidi nitaonyesha mazuri zaidi ya haya.”

Mabao hayo yamemfanya Mudathir kufikisha jumla ya mabao matatu kwenye msimu wa ligi, jingine alitupia wakati Azam FC ikiilaza Mbeya City 2-1 huku akiwa na bao moja katika michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) alilofunga walipoichapa African Lyon 4-0.