MABAO mawili yaliyofungwa na kiungo wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Mudathir Yahya ‘Muda’, kwenye ushindi wa 2-0 yametosha kabisa kuiua Majimaji ya Songea ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni ya leo.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) wakiishusha Simba yenye pointi 57 baada ya kufikisha jumla ya pointi 58 huku Yanga nayo iliyoshinda 2-1 dhidi ya Mgambo JKT ikiwa kileleni kwa kujikusanyia pointi 62.

Mchezo huo wa leo ulikutanisha makocha waliowahi kufanya kazi pamoja Azam FC misimu iliyopita, kocha wa sasa Stewart Hall na Msaidizi wake wa zamani ambaye ni Kocha Mkuu wa Majimaji, Kally Ongalla, aliyeiongoza timu hiyo kutopoteza mchezo wowote ndani ya mechi nane zilizopita kabla ya rekodi hiyo kustopishwa leo.

Azam FC ililazimika kusubiri hadi kipindi cha pili kuweza kuandikisha ushindi huo baada ya kufanya mabadiliko ya kumwingiza mshambuliaji Ame Ally ‘Zungu’ na kupumzishwa mfungaji bora wa timu hiyo msimu uliopita Didier Kavumbagu.

Kuingia kwa Zungu kuliiweka katika wakati mgumu safu ya ulinzi ya Majimaji chini ya wakongwe Godfrey Taita, Alex Kondo na Lulanga Mapunda, ambayo ilishindwa kuhimili kasi ya mashambulizi ya Azam FC na kujikuta ikiruhusu mabao mawili ndani ya dakika 12.

Bao la kwanza likifungwa dakika ya 51 na Mudathir aliyeunasa mpira uliokoswa na Zungu kufuatia krosi ya Ramadhan Singano ‘Messi’ na kupiga shuti lililomshinda kipa wa Majimaji, David Buruani.

Alikuwa ni Mudathir tena dakika ya 63 aliyemtungua kwa mara nyingine Buruani kwa kupiga shuti zuri akitumia vema pasi ya Khamis Mcha ‘Vialli’, aliyewalamba chenga mabeki wawili wa Majimaji na kutoa pande safi kwa mfungaji huyo.

Mabao hayo yamemfanya Mudathir kufikisha bao la nne msimu huu, matatu akifunga kwenye ligi na moja akitupia katika Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) wakati Azam FC ikitinga hatua ya 16 bora kwa kuichapa African Lyon iliyorejea Ligi Kuu kwa msimu ujao mabao 4-0.

Yawakosa nyota wake nane

Azam FC iliyoshindwa kucheza vema kipindi cha kwanza, iliingia katika mchezo huo ikiwa na mapengo ya kutokuwepo kikosini kwa wachezaji wake nane wa kikosi cha kwanza waliokosekana leo kwa matatizo tofauti.

Mabeki Shomari Kapombe, Pascal Wawa, Wazir Salum, Racine Diouf, viungo Frank Domayo, Michael Bolou na  mshambuliaji Kipre Tchetche, wenyewe ni wagonjwa huku kiungo mkabaji Himid Mao akikosekana kwa kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar.

Hali hiyo iliilazimu benchi la ufundi la Azam FC kuwaorodhesha kwenye kikosi wachezaji wawili kutoka academy ya timu hiyo, kiungo na nahodha wa Azam FC Academy, Abdallah Masoud ‘Cabaye’ na mshambuliaji Shabaan Idd, aliyefanikiwa kucheza dakika sita za mwisho za mchezo huo akichukua nafasi ya Mcha ‘Vialli’.

Vikosi vilivyocheza leo:

Azam FC: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael/Abdallah Kheri dk 74, David Mwantika, Aggrey Morris, Jean Mugiraneza, Salum Abubakar, Ramadhan Singano, Mudathir Yahya, Khamis Mcha/Shabaan Idd dk 84, Didier Kavumbagu/Ame Ally dk 46

Majimaji: David Buruani, Godfrey Taita, Mpoki Mwakinyuke, Bahati Yusufu, Lulanga Mapunda, Alex Kondo/Samir Luhava dk 86, Peter Mapunda/Paul Maona dk 58, Hassan Khamis, Danny Mrwanda, Luka Kikoti/Iddy Kipagwile dk 68, Marcel Bonaventure