WINGA chipukizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid Mussa, aliyeko majaribioni nchini Hispania, jana aliiongoza CD Tenerife ya Ligi Daraja la Kwanza nchini humo ‘Segunda Division’ kuichapa UD Diabora bao 1-0.

Habari njema zaidi kuhusu Farid ni winga huyo kufanya vizuri katika mtihani wake huo wa kwanza baada ya kuwapagawisha viongozi na benchi la ufundi la Tenerife.

“Naendelea vizuri sana na jana usiku nilicheza dakika 45 katika mchezo wa kirafiki na nimeiongoza timu hiyo kupata ushindi, nimefanikiwa kuivutia hii timu kwani walishangazwa na kiwango changu kizuri hadi kudiriki kuniuliza kama kweli mimi ni Mtanzania baada ya mechi hiyo,” alisema Farid wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Kwa mujibu wa wakala wa Farid, John Sorzano raia wa Venezuela aliyeishi sana nchini England, amedai kuwa wiki ijayo nyota huyo anatarajia kuanza rasmi majaribio katika timu mbili za Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ akianzia Las Palmas na kumalizia Malaga.

Farid atafanya majaribio hayo na kukaa huko kwa wiki mbili zijazo akitarajiwa kurejea nchini Mei 19 mwaka huu wakati msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakapokuwa umemalizika.

Lakini mechi pekee ambayo anaweza kuiwahi ni ile ya fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) itakayofanyika Mei 25 mwaka huu, ambayo Azam FC ilitinga juzi kwa kuichapa Mwadui ya Shinyanga na itacheza na mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Yanga na Coastal Union.