KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa yupo tayari kucheza mchezo wa fainali wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya timu yoyote atayopangiwa nayo ikiwemo kutwaa taji la michuano hiyo.

Azam FC juzi ilifanya makubwa kwa kutinga fainali ya kwanza ya michuano hiyo tokea iliporejeshwa tena msimu huu baada ya kukosekana kwa miaka 14, ikiichapa Mwadui ya Shinyanga kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia dakika 120 kuisha kwa sare ya mabao 2-2.

Mabingwa hao wanaodhaminiwa na Benki ya NMB, wanasubiria kujua ni timu gani watakayocheza nayo kwenye fainali hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Mei 25 mwaka huu, hii ni baada ya mchezo wa nusu fainali nyingine kuvunjika kufuatia vurugu kubwa iliyotokea ndani ya Uwanja wa Mkwakwani Tanga, wakati huo Yanga alikuwa mbele kwa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Hall alisema kuwa bado wanasafari ndefu kuelekea mchezo huo wa fainali na kudai kuwa kwa sasa mawazo yake yote yapo katika mechi sita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) zilizobakia kwa kuhakikisha anashinda zote.

“Tulikuwa na matatizo mengi tulivyocheza na Mwadui, kwanza kuna wachezaji walikuwa na homa, wengine majeruhi na uchovu wa safari ndefu kutoka Tunisia na hatukupata muda mzuri wa kupumzika, hiyo iliathiri kiwango chetu jana (juzi) na hata mimi sikufikiria kama tunaweza kuonyesha kiwango bora katika mchezo huo hasa kutokana na matatizo hayo, Mwadui wenzetu walikuwa na muda mrefu wa kujiandaa na nilitarajia wangeonyesha kiwango hicho.

“Malengo tuliyojiwekea katika mchezo huo ni kila mmoja kutimiza majukumu yake vema ipasavyo katika eneo lake jambo ambalo tulifanikiwa, lakini kama sio umiliki mpira kupungua katika eneo la kiungo kuelekea mwishoni mwa mchezo huo tungeimaliza mechi mapema kwa kupata ushindi wa bao 1-0 na tusingefika muda wa dakika za nyongeza, hata baada ya dakika hizo mechi ilitakiwa kuisha kwa ushindi wa 2-1 kama sio ubovu wa waamuzi,” alisema.

Ashangazwa na mwamuzi

Hall aliendelea kushangazwa na maamuzi ya waamuzi wengi wanaochezesha mechi zao msimu huu, hasa baada ya juzi mwamuzi Andrew Shamba kutoka mkoani Pwani kuipa penalti ya utata Mwadui kwenye dakika za mwisho za nyongeza iliyopelekea mchezo huo kuamuriwa kwa hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti.

“Waamuzi wengi kuvurunda kwenye mechi zetu imeuwa ikiwapa presha sana wachezaji wangu na kutoka nje ya mchezo, sisi kufika hatua ya penalti ilikuwa ni utani, sio tu utani bali mwamuzi alisababisha hilo na hii ni baada ya kutoa penalti isiyo halali tena wakati muda wa dakika tano za nyongeza zilizoongezwa ukiwa umezidi…Kwa mara nyingine tunaongelea waamuzi, waamuzi na tunashindwa kuongelea mpira, hii sio kitu kizuri kwenye soka la Tanzania,” alisema

Aliongeza kuwa: “Nimefurahishwa sana na matokeo tuliyopata, wachezaji wangu wamepigana kwa nguvu na kufanya kazi kwa bidii kwenye mchezo huo, lakini kutokana na waamuzi tumemaliza mechi tukiwa na kadi nyekundu, unajua tumepata kadi za njano na nyekundu kutokana na waamuzi kuwachanganya wachezaji wetu jambo ambalo linachukiza, tumepata matokeo tuliyoyataka lakini tunamkosa David (Mwantika) katika fainali kwa sababu amefungiwa.”

Tuna nafasi mbili CAF

“Kwa sasa baada ya kuingia fainali tumejihakikishia nafasi mbili za kushiriki michuano ya Kimataifa mwakani, tunachoangalia hivi sasa ni kushinda mechi zetu sita za ligi zilizobakia hiyo itatupa nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi huku pia tukitakiwa tushinde mchezo huo wa fainali,” alisema Hall.

Mfumo unambeba Mcha

Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ na Sofapaka ya Kenya, amefurahishwa na kiwango kizuri kinachoendelea kuonyeshwa na mshambuliaji wake Khamis Mcha ‘Vialli’, aliyefunga mabao mawili pekee ya Azam FC katika mchezo huo.

“Amefunga mabao matatu sasa katika mechi nne zilizopita, kwa sasa hatuutumii mfumo wa 3-5-2 ambao umekuwa hauendani naye, kutokana na kutokuwa na uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa pembeni mwenye kazi nyingine ya kuwa kama winga (wingbacks), kwa sababu sio mtu wa ulinzi, hivi sasa tunatumia mifumo miwili 4-3-3 na 3-5-2 tukiwa tunaibadilisha mara kwa mara, Mcha anaendana sana na mfumo wa 4-3-3 na kila tunapoutumia amekuwa akifunga mabao.

“Tumefurahishwa naye sana kwa sababu ni mchezaji mzuri sana kuanzia mazoezini, pia ni kijana profesheno na hata asipokuwepo kikosini amekuwa akifanya kazi kwa nguvu na bidii zaidi, kiukweli amenifurahisha sana,” alisema.

Mipango mchezo vs Majimaji

Kocha huyo raia wa Uingereza, alisema kuwa kwa maa nyingine hawapati nafasi ya kupumzika baada ya kumaliza mchezo wa Mwadui kwani wanatakiwa kucheza na Majimaji kesho Jumatano katika mechi ya ligi itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kabla ya Jumapili ijayo kukipiga na Simba Uwanja wa Taifa.

“Sisi hatupumziki, unajua Majimaji imepumzika, Simba nayo imepumzika vizuri na inatusubiria sisi, Majimaji ipo kwa takribani wiki moja sasa Dar es Salaam wakijiandaa dhidi yetu, wachezaji wangu wamechoka, kwa sasa ziwezi kufikiria kikosi kitakachocheza dhidi ya Majimaji kwa sababu wachezaji wangu wengine ni wagonjwa, Bolou (Michael) na Racine (Diouf) wana homa, Domayo (Frank) majeruhi na hatujui kama atakuwepo siku hiyo, bado tunawakosa Wawa (Pascal), Kapombe (Shomari), Tchetche (Kipre), Farid (Mussa) ameenda Hispania, Himid (Mao) ana kadi nyekundu.

“Hivyo tunajua namna ya kucheza mchezo huo, lakini itakuwa fursa nyingine kumuona zaidi Mcha akicheza na Mudathir (Yahya) pia, ila tutajua wachezaji watakaokuwa fiti mara baada ya mazoezi ya kesho (leo) jioni, tutakapoanza maandalizi hayo,” alisema.

Azam FC iliyotwaa ubingwa wa ligi msimu wa 2013/14 kwa rekodi ya aina yake ya kutofungwa mchezo wowote, kwa sasa imejikusanyia jumla ya pointi 55 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo lakini imezidiwa mchezo mmoja na Simba iliyonfasi ya pili wakiwa na pointi 57 huku Yanga ikiwa kileleni wakijizolea pointi 59.