MFUNGAJI wa mabao mawili ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Khamis Mcha ‘Vialli’, kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mwadui ya Shinyanga amemzawadia mchumba’ke, Thureya Khamis.

Mabao hayo ya Mcha yalichangia Azam FC kutinga fainali ya michuano hiyo jana jioni baada ya dakika 120 kuisha kwa sare ya  2-2 kabla ya mabingwa hao kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-3.

Hata hivyo Mcha alishindwa kuendelea na mchezo huo kufuatia kupata maumivu madogo ya mguu na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji Allan Wanga.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Mcha alisema mchumba wake huyo aliyezaa naye watoto watatu ndio kila kitu kwake, huku akidai kuwa mabao hayo yamezidi kumwongezea nguvu zaidi kuelekea mechi zijazo katika kuing’arisha zaidi Azam FC.

“Kwanza namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kumaliza mechi salama kwa sisi kuibuka na ushindi, haikuwa mechi rahisi Mwadui ilipambana nayo ikitaka kuingia fainali ili iweze kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani, kikubwa tulichokizingatia ni umuhimu wa mechi hasa ikizingatiwa hatukufanya vizuri Tunisia, hivyo leo (jana) ilikuwa ni nafasi yetu ya kuendelea kushiriki michuano ya Kimataifa mwakani,” alisema.

Mcha aliyeanza kurejesha makali yake ya msimu uliopita baada ya kupona majeraha ya goti yaliyokuwa yakimsumbua, alisema kuwa anajisikia furaha sana kufunga mabao hayo mawili, pia wachezaji wenzake nao wamefurahia ushindi huo, ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wengi wa Azam FC waliokuwa na uchu wa kuiona timu hiyo ikitinga fainali itakayofanyika Mei 25 mwaka huu na kutwaa taji hilo.

“Hakuna jambo lolote kubwa ni mpira tu, inatokea mtu akifanya makosa unatumia vema kama nilivyofunga mimi, mipango mingine anatuelekeza kocha na mambo mengine sisi wachezaji huongeza wenyewe kwa juhudi binafsi, mabao hayo yamenipa morali sana kwa ajili ya mechi ya fainali na hata mechi nyingine za ligi zinazokuja, ninaimani Mungu akipenda na kunipa uzima zaidi nitaweza kufanya vizuri zaidi na kuisadia timu yangu,” alisema.

Mabao hayo yamemfanya Mcha kufikisha jumla ya mabao matatu msimu huu yote akifunga katika michuano hiyo, ambapo moja jingine alitupia wakati Azam FC ilipotinga nusu fainali kwa kuichapa Tanzania Prisons mabao 3-1.