KIPA namba moja wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aishi Manula, anajisikia furaha kubwa kuipeleka timu hiyo kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuitoa Mwadui katika nusu fainali ya michuano hiyo iliyofanyika Uwanja wa Mwadui, Shinyanga jana jioni.

Aishi anafuraha hiyo kufuatia kupangua mkwaju wa penalti wa nne wa Mwadui uliopigwa na mshambuliaji Kelvin Sabato kabla ya beki Aggrey Morris kufunga penalti ya mwisho iliyoifanya timu hiyo kushinda kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia dakika 90 na 30 za nyongeza kuisha kwa sare ya mabao 2-2.

Mabao yote ya Azam FC yakifungwa na Khamis Mcha ‘Vialli’ huku yale ya Mwadui yakipigwa na Salum Kabunda na Jabir Azizi aliyefunga kwa mkwaju wa penalti.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Aishi alisema anajisikia vizuri kuokoa penalti hiyo, huku akidai kuwa wao kama wachezaji walikuwa na malengo ya kushinda nusu fainali hiyo, jambo ambalo walifanikiwa na kutinga fainali hiyo.

“Sisi kama wachezaji nia yetu ilikuwa ni kufika fainali na kuchukua kombe, kwa hiyo ili uchukue kikombe lazima ufike fainali.

“Kwa hiyo mimi binafsi nina furaha tumeweza kufika fainali, Inshallah Mungu akijalia tutafikia malengo, nadhani mchezo wa fainali tutajiandaa kwa sababu tuna muda wa kujiandaa na kuweza kufanya vizuri,” alisema.

Aishi amekuwa kwenye kiwango bora sana hivi sasa kwani mpaka sasa ameshadaka penalti tatu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mwadui, Yanga na Kagera Sugar.

Kiwango hicho bora kimetosha kabisa kumfanya Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa, amuamini kwa kumchezesha kama kipa namba moja kwenye kikosi chake katika mechi za hivi karibuni.