NAHODHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao, amewafuta machozi wote wa timu hiyo baada ya kutolewa jana na Esperance ya Tunisia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Himid aliyeingia dakika ya 79 katika mtanange huo kuchukua nafasi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’, amewaambia mashabiki hao kuwa kwa sasa nguvu zao zote wanahamishia katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) akiwaaidi kuwa watapambana kuchukua makombe yote hayo.

“Matokeo yamewasikitisha watu wengi hata sisi wachezaji, lakini wanatakiwa wajue Azam FC ni timu changa sana na kwa sasa tunapiga hatua kubwa lakini hii haitufanyi tuvimbe vichwa kwani bado tuna deni, hivyo nafikiri inabidi tufanye kitu kikubwa zaidi kuweza kusogea na wao mashabiki waendelee kutupa sapoti bado ligi ipo, FA ipo tutajitahidi kuweza kuchukua makombe yote hayo,” alisema Himid wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, imeondolewa kwenye michuano hiyo baada ya kufungwa mabao 3-0 jijini Rade jana na hivyo waarabu hao kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2 kutokana na ushindi wa awali wa 2-1 jijini Dar es Salaam iliyoupata matajiri hao wa Azam Complex.

“Mchezo ulikuwa mgumu, ulikuwa mzuri dakika 45 za kipindi cha kwanza tuliweza kuikabili presha ya ugenini na hatukuweza kuruhusu bao, kipindi cha pili naona wenzetu walirudi na nguvu zaidi, tulizuia wakapata mabao kutokana na labda makosa yetu ya kiuchezaji wakaweza kushinda mchezo,” alisema.

Mafundisho waliyopata

Himid alisema kuwa ni hatua kubwa wamefikia mpaka sasa hadi kutolewa hasa kutokana na ukubwa wapinzani wao waliokuwa wakipambana nao.

“Unajua mpira ni mchezo wa makosa na katika mpira unajifunza kila siku iwe unacheza mechi au unafanya mazoezi, ukiiangalia Esperance ipo kwenye nafasi za juu Afrika (nafasi ya tatu), ni timu nzuri ni timu bora, sisi kufika hapa na namna tulivyocheza na hatua kubwa sana tumefika lakini ni changamoto kwetu inabidi tuchukue kitu kutoka leo (jana), ambacho kitatusaidia kufanikiwa katika mashindano yanayokuja mbele,” alisema.

Azam FC iliyopanda Ligi Kuu miaka nane iliyopita, msimu huu ilikuwa ikishiriki kwa mara ya nne michuano ya Afrika hadi inafika raundi hiyo ilifanikiwa kuwatoa Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 7-3.