KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa kikosi chake kimetolewa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na timu bora barani humo ya Esperance ya Tunisia, licha ya kikosi chake kufanya baadhi ya makosa mchezoni jana.

Mchezo huo wa marudiano wa raundi ya pili ya michuano hiyo ulifanyika katika Uwanja wa Olimpique de Rades na wenyeji Esperance kushinda kwa mabao 3-0 na hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 4-2 kutokana na Azam FC kushinda 2-1 jijini Dar es Salaam siku 10 zilizopita.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz leo mara baada ya mazoezi ya timu hiyo kwenye ufukwe wa Hoteli waliyofikia ya El Mouradi Gammarth, Hall alisema kuwa Esperance walicheza vizuri kwenye mchezo huo hususani kipindi cha pili na makosa waliyofanya baada ya kuanza kipindi hicho yamewafanya wapinzani wao kupata ushindi huo.

“Tulifanya baadhi ya makosa lakini tunatakiwa kuweka sawa hilo suala kwenye uwiano kwa sababu huko nyuma nilisema Esperance ni timu namba tatu kwa ubora Afrika sisi wa 345, Esperance ilicheza vizuri sana wakati mwingine unapopoteza hutakiwi tu kuangalia makosa yako lazima uangalie pia ubora wa wapinzani wako.

“Usiku wa jana Esperance ilicheza vizuri sana hasa kipindi cha pili, walicheza kwa haraka na soka la kushambulia zaidi wakiwa na wachezaji wazuri sana na kusababisha madhara kwetu, kama ukiangalia kwa mtazamo mkubwa utagundua kuwa kabla ya kufungwa bao la tatu tulikuwa na nafasi ya kuushinda mchezo, kwa jumla ya dakika 117 (pamoja na mchezo wa Dar es Salaam) tulifanikiwa kuwa vizuri lakini baada ya hapo tuliweza kufanya makosa,” alisema.

Aishi kipa bora

Hall alisema licha ya Aishi Manula kufanya makosa mawili ya kiufundi yaliyowapa mabao wapinzani wao, anaamini ya kuwa huyo ni kipa bora zaidi anayechipukia kwani alifanikiwa kuokoa hatari nyingi sana hasa kipindi cha kwanza kwa kuwanyima mabao ya wazi Esperance.

“Kosa la kwanza alilifanya kwenye bao la kwanza, alikaa pembeni kidogo ya ukuta wakati mpira wa adhabu unapigwa hata alipougusa mpira na vidole ili autoa alishindwa kutokana na hilo, bao la pili aliudaka mpira wa krosi na kuuachia na kufungwa.

“Lakini ni kipa chipukizi ambaye bado anajifunza zaidi, ni kipa mzuri kipindi cha kwanza aliokoa nafasi nyingi za Esperance kufunga hata kipindi cha pili lakini alifanya makosa madogo ambayo si tatizo,” alisema.

Kushindwa kumiliki mpira

“Udhaifu mwingine ambao tumeufanya ni kushindwa kupoteza sana mipira, unapocheza na timu nzuri unapopata mpira lazima uulinde na kukaa nao kwa sababu unaposhindwa kukaa nao unampa mpinzani wako nafasi ya kukushambulia kwa nguvu, unatakiwa kumiliki mpira ili kuua kasi ya mchezo na pia kupumzika, huwezi mwanzo hadi mwisho ni kuzuia kuzuia, nafikiri jana tulifanya kazi kubwa ya kuupata mpira lakini tulishindwa kukaa nao,” alisema.

Kocha huyo raia wa Uingereza alisema kuwa kuna baadhi ya mambo wanatakiwa kuboresha ili kufanya vizuri kwa baadaye na kudai kuwa juhudi kwenye timu ipo vizuri mipango yao ya kipindi cha kwanza ilienda vizuri, lakini kuna baadhi ya wachezaji wanatakiwa kujifunza namna ya kucheza kwa dakika zote 90 kwa ubora ule ule.

Mabao matatu Dar yangetubeba

Hall alizungumzia ushindi kiduchu wa mabao 2-1 walioupata kwenye mchezo wa kwanza na kupoteza nafasi nyingi akidai kuwa: “Hilo nalo ni tatizo tulilolion usiku wa jana, tulitakiwa kupata bao la tatu Dar es Salaam kama tungepata bao hilo jana ingekuwa ni presha zaidi kwao, tulipopata ushindi wa 2-1 na wao kupata bao la ugenini, walihitaji ushindi wa bao 1-0 ili kusonga mbele, jambo ambalo lilituweka kwenye wakati mgumu sisi, hivyo tulihitaji kufunga bao la tatu Dar es Salaam.”

Fundisho walilopata msimu huu

Akizungumzia fundisho walilopata msimu kwenye michuano hiyo ya kimataifa, Hall alisema: “Wachezaji wengi waliocheza kwenye mchezo dhidi ya timu hii kucheza dakika zote 90 imekuwa ni shida, jambo lililoonekana kwenye mchezo wa jana, tuliweza kucheza kwa kiwango chetu kwa saa moja, lakini baada ya hapo walikuwa bora zaidi yetu, lakini naweza kusema kuwakosa wachezaji wetu wanne tegemeo nalo limetufanya tuwe kwenye wakati mgumu zaidi.”

Wachezaji hao wanne wa Azam FC waliokosekana na jana, ni mabeki Pascal Wawa, Shomari Kapombe na mshambuliaji Kipre Tchetche, ambao wote ni wagonjwa huku kiungo mkabaji Jean Baptiste Mugiraneza aliikosa kutokana na kutumikia adhabu ya kukusanya kadi mbili za njano.

Changamoto za FA Cup, VPL

Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ na Sofapaka ya Kenya, alisema kuwa kabla ya mazoezi ya leo ufukweni, amewaambia wachezaji wake kuwa wasahau yaliyopita sasa wafikirie mechi zao nane zilizobakia katika Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ili kufanya vizuri.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, Jumapili ijayo Aprili 24 itakuwa na mchezo mgumu wa nusu fainali ya FA Cup watakaocheza ugenini dhidi ya Mwadui ya mkoani Shinyanga kabla ya siku tatu baadaye (Aprili 27) kukipiga na Majimaji katika mechi ya ligi itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex.

“Nimewaambia lazima tujipange vema kwa michuano miwili hiyo tuliyobakiwa nayo, kwa sababu tunataka kujaribu kushinda makombe yote hayo tuliyobakiwa nayo jambo ambalo tunaweza, tmebakiwa na mechi nane hivyo tunatakiwa kuhakikisha tunashinda mechi zote, jambo zuri zaidi Kipre, Wawa, Migi wanarejea kikosini, bado tutaendelea kuwa bila Kapombe, hivyo kama una wachezaji watatu wanarejea na wachezaji wengine wako fiti kikosi kinarejea kuwa na nguvu yake,” alisema.

Hall alisema kuwa ratiba ya kikosi hicho kitakachorejea jijini Dar es Salaam Ijumaa saa 9 Alasiri, itakuwa ni kupitiliza moja kwa moja mkoani Mwanza kwa usafiri wa ndege kabla kupumzika mkoani humo na baadaye kuwafuata Mwadui kwa ajili ya kukipiga nao siku mbili zinazofuata.