NDOTO za Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika zimefutika baada ya jana kufungwa na Esperance ya Tunisia mabao 3-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Olympique de Rades.

Azam FC kupoteza mchezo huo wa marudiano wa raundi ya pili ya michuano hiyo, kumeifanya itoke kwa kufungwa jumla ya mabao 4-2 na hii ni kufuatia awali timu hiyo kushinda 2-1 kwenye mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam.

Mabingwa hao wa michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) waliingia kwenye mchezo huo wa marudiano, wakiwakosa nyota wake wanne wa kikosi cha kwanza, mabeki Pascal Wawa, Shomari Kapombe, mshambuliaji Kipre Tchetche, ambao wote hao walishindwa kusafiri na timu kutokana na kuwa wagonjwa

Nyota mwingine wa nne aliyeukosa mchezo huo ni kiungo Jean Mugiraneza ‘Migi’, aliyekuwa akitumikia adhabu ya kukusanya kadi mbili za njano kwenye michuano hiyo.

Kwa ujumla Azam FC ilifanikiwa kuwadhibiti vema Esperance, licha ya presha kubwa ya mashambulizi iliyokuwa ikielekezwa langoni mwao na shukrani ziende kwa kipa Aishi Manula, aliyeokoa michomo mingi ya nguvu ya wapinzani wao.

Hivyo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu yoyote iliyoweza kuona lango la mwenzake, ambapo baada ya kurejea kipindi cha pili Esperance ilionekana kuendeleza kasi ya kusaka bao.

Dakika ya 46 mwamuzi wa mchezo huo, Redouane Jiyed, aliingia kwenye mtego wa kudanganywa na winga wa Esperance, Fakhreddine Ben Youssef, aliyejidondosha nje kidogo ya eneo la 18 wakati alipopokonywa mpira na kiungo Frank Domayo na mwamuzi huyo kuamuru ipigwe faulo kuelekea langoni mwa Azam FC, ambayo ilifungwa kiufundi na Saad Bguir.

Mshambuliaji wa Esperance Haythem Jouini, alitumia uzembe uliofanywa na kipa wa Azam FC, Aishi Manula, dakika ya 63 ya kuutema vibaya mpira wa krosi uliochongwa na nahodha wake, Hocine Ragued, na kuuwahi mpira huo kwa kupiga kichwa kilichojaa wavuni.

Benchi la Ufundi la Azam FC lilifanya mabadiliko dakika ya 65 kwa kumpumzisha winga teleza Farid Mussa, aliyetonesha majeraha ya enka na kuingia Khamis Mcha, dakika ya 79 yalifanywa maadiliko mengine mawili kwa kutoka kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na beki Wazir Salum na nafasi zao kuchukuliwa na Didier Kavumbagu na Himid Mao.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ilijitahidi kushambulia kutafuta bao na sekunde chache baada ya mabadiliko hayo nahodha John Bocco, alipiga shuti kali pembezoni mwa uwanja liliokolewa vema na kipa wa Esperance,  Moez Ben Cherifia na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Esperance ilifanya shambulizi la kushtukiza dakia ya 80 kwa kugongena pasi kadhaa na alikuwa ni Youssef aliyeitimisha ushindi wao huo kwa kufunga bao la tatu kwa shuti akimalizia pasi nzuri na Jouini, aliyeipiga pembeni ya uwanja kabla ya winga huyo kukutana nayo na kufunga.

Kuelekea mwishoni mwa mchezo huo iliwabidi Jeshi la Polisi la hapa liwatawanye mashabiki waliokuwa kwenye jukwaa la nyuma ya lango la Azam FC baada ya kuwabuguzi wachezaji wa timu hiyo huku wengine wakimmulika machoni na miale ya mwanga kipa Aishi Manula.

Hadi dakika 90 zinamalizika walikuwa ni Esperance walioibuka na ushindi huo na kusonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano, watakapokutana na moja ya timu iliyotolewa katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kupitia droo itakayofanyika kesho Alhamisi jijini Cairo, Misri, ikipenya tena hapo itaingia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa;

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Wazir Salum/Himid Mao dk 79, David Mwantika, Aggrey Morris, Michael Bolou, Ramadhan Singano, Frank Domayo, John Bocco, Salum Abubakar/Didier Kavumbangu dk 79, Farid Mussa/Khamis Mcha dk 65.