BARABARA ya Kijiji cha Mvomero, mkoani Morogoro ililazimika kutopitika kwa takribani dakika 15 kufuatia mashabiki wa soka wa kijiji hicho kujazana kwa wingi na kufunga barabara hiyo wakati wakiipokea Azam FC iliyotoka kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0 kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) jana jioni.

Tukio hilo lilitokea saa 1 usiku wakati kikosi cha Azam FC kilipokuwa kikishuka kwenye basi dogo la timu kuelekea kupanda basi kubwa la timu lililokuwa limepaki kwenye Kituo Kidogo cha Polisi cha Mvomero.

Azam FC ililazimika kuondoka na basi dogo la timu kutokea hapo Mvomero kutokana na miundombinu mibovu ya barabara kuelekea kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, hivyo mashabiki hao takribani 100 waliochanganyika rika na jinsia zote walilazimika kusubiria kwa takribani saa mbili hadi kikosi hicho kiliporejea tena hapo kupanda basi hilo kubwa mara baada ya mchezo huo.

Mara baada ya Azam FC kuwasili hapo mashabiki hao walishangilia kwa nguvu na kuwapongeza wachezaji kila walipopita na kupelekea magari yaliyopita njia hiyo kusimama na kusubiria tukio hilo liishe kutokana na kuwa na msongamano wa watu wengi walioziba barabara.

Mashabiki wengine waliokuwa na baiskeli na pikipiki walidaiwa kutokea vijiji vya karibu na hapo ili kuwaona nyota wa Azam FC watakapokuwa wakiwasili eneo hilo kupanda basi hilo na hata lilipoondoka kila sehemu timu hiyo ilipopita mashabiki walisikika kupiga miluzi na kuita majina ya baadhi ya wachezaji akiwemo John Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga bao hilo pekee jana.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB mpaka sasa imekuwa ikijizolea mashabiki wengi katika sehemu mbalimbali nchini kutokana na namna inavyoendesha timu kisasa na matokeo mazuri wanayopata uwanjani kwenye ligi na michuano ya Kimataifa.