KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imezidi kufufua matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0 katika Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro jioni ya leo.

Ushindi huo wa Azam FC umekuja wakati ikitoka kupata sare mbili mfululizo kwenye mechi zilizopita za ligi dhidi ya Toto Africans (1-1) na Ndanda (2-2).

Shukrani za kipekee ziende kwa nahodha John Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga bao hilo pekee kwa njia ya mkwaju wa penalti na kuihakikishia Azam FC pointi zote tatu muhimu ugenini.

Kikosi cha Azam FC kwa mara ya kwanza kwenye ligi, leo kilikuwa bila beki kisiki Pascal Wawa, ambaye amekusanya kadi tatu za njano na akiwa katika programu ya kuwekwa fiti kwa ajili mchezo ujao dhidi ya Esperance, nafasi yake ilichukuliwa na Racine Diouf.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kwa pande zote mbili kushambuliana kwa zamu, lakini kwa kiasi kikubwa mipango yao ilikuwa ikiharibika kila walipopiga pasi fupi kutokana na uwanja kujaa maji katika baadhi ya maeneo uwanjani.

Hivyo timu zote zililazimika mara nyingi kutumia mipira mirefu katika kushambulia hali iliyofanya mara nyingi mpira kuchezwa sana katikati ya uwanja.

Dakika ya 16 beki wa Mtibwa Sugar, Andrew Vincent ‘Dante’ alifanya kazi ya ziada kuinyima bao Azam FC baada ya kuokoa mpira kwenye mstari kufuatia kichwa kilichopigwa na Bocco, aliyetumia uzembe wa kipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed aliyeuokoa vibaya mpira wakati akiruka naye juu.

Mabingwa hao wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), wangeweza kuondoka na mabao mawili kipindi cha kwanza kama wachezaji wake Kipre Tchetche na beki Racine Diouf wangekuwa makini kutumia nafasi walizopata na hivyo hadi mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana.

Kipindi cha pili kilianza kwa benchi la ufundi la Azam FC chini ya Stewart Hall, kufanya mabadiliko ya kutoka Diouf na nafasi yake kuchukuliwa na Abdallah Kheri, lengo likiwa ni kuimarisha eneo la ulinzi.

Dakika ya 61 Tchetche alifanya kazi ya ziada kumkimbiza Andrew Vincent ‘Dante’ wa Mtibwa Sugar na kupiga krosi ya hatari pembeni kidogo ya eneo la 18 na beki huyo alijikuta akiunawa mpira huo katika harakati za kuokoa na mwamuzi Alex Mahagi kutoka Mwanza kuamuru penalty ipigwe langoni mwa Wakata miwa hao.

Alikuwa ni nahodha Bocco aliyefunga kiustadi penalti hiyo na kufikisha bao la tisa msimu huu akimfikia staa mwingine wa kikosi hicho Tchetche, ambaye alipumzishwa dakika 79 baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Allan Wanga.

Azam FC ilifanya mabadiliko mengine dakika tatu baadaye baada ya kiungo Michael Bolou, kupata majeraha madogo na nafasi yake ikachukuliwa na kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kukaba Jean Baptiste Mugiraneza.

Katika hali ambayo haikutarajiwa dakika ya 90 mwamuzi Mahagi alimuonyesha kadi nyekundu kiungo wa Azam FC, Himid Mao.

Himid alipata kadi hiyo ikiwa ni baada ya kumuonyesha mwamuzi kutokukubaliana na namna alivyofanyiwa na watu wa huduma ya kwanza waliompandisha vibaya kwenye machela wakati wakimtoa nje uwanja kutibiwa kufuatia kudondoka chini alipopigwa usoni na mchezaji wa Mtibwa Sugar.

Hata hivyo, hadi mpira huo unamalizika ni Azam FC iliyoondoka kifua mbele na ushindi huo umeifanya kufikisha jumla ya pointi 55 katika nafasi ya tatu, ikizidiwa pointi mbili na Simba inayoongoza kileleni na pointi moja dhidi ya Yanga, ambayo ipo nyuma mchezo mmoja.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho saa 1 asubuhi na wachezaji watapewa mapumziko ya siku moja kabla ya keshokutwa kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo ujao wa marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance utakaofanyika jijini Tunis Aprili 19 mwaka huu.  

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Wazir Salum, David Mwantika, Aggrey Morris, Racine Diouf/Abdallah Kheri dk 46, Himid Mao, Michael Bolou/Jean Mugiraneza dk 82, Frank Domayo, Ramadhan Singano, John Bocco, Kipre Tchetche/Allan Wanga dk 79