KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kimeanza safari saa 7.00 mchana huu wa leo kuelekea mkoani Morogoro kwa ajili ya kupambana na Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika kesho Jumatano saa 10.30 jioni.

Azam FC imeondoka ikiwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi na kurejesha matumaini ya kutwaa ubingwa wa ligi baada ya kutoka sare katika mechi mbili zilizopita za ligi dhidi ya Toto Africans (1-1) na Ndanda (2-2).

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa wanajua ya kuwa mchezo huo utakuwa mgumu, lakini wamejipanga kuondoka na ushindi.

“Tumecheza mara mbili na Mtibwa Sugar kwenye mechi zilizopita moja tumeshinda (1-0) na nyingine iliisha kwa sare katika Kombe la Mapinduzi (1-1), natarajia mchezo mgumu, lakini tmejipanga kuibuka ushindi,” alisema.

Wawa, Sure Boy nje

Hall alisema kuwa katika mchezo huo anatarajia kuwakosa nyota wake watatu, mabeki Pascal Wawa, Shomari Kapombe na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambao wote ni wagonjwa huku sababu nyingine inayomweka Wawa nje ikiwa ni kukusanya kadi tatu za njano.

“Wawa na Sure Boy watabaki Dar es Salaam kupata tiba ya kuwaweka sawa chini ya Mtaalamu wa Viungo na Tiba, Adrian Dobre, lengo ni waiwahi mechi ya marudiano dhidi ya Esperance jijini Tunis, licha ya kuwakosa hao bado tuna kikosi kizuri kwani David Mwantika atachukua nafasi ya Wawa,” alisema.

Kikosi cha Azam FC kinaelekea huko kikiwa tayari kimejikusanyia jumla ya pointi 52 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 23, ikishinda 15, sare saba na kufungwa mchezo mmoja.