KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imepangwa kucheza na Mwadui katika nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), mchezo uliopangwa kufanyika Uwanja wa Mwadui, Shinyanga Aprili 24 mwaka huu.

Mchezo mwingine wa nusu fainali utakaopigwa siku hiyo, utazihusisha Coastal Union kutoka jijini Tanga itakayowakaribisha Yanga ndani ya Uwanja wa Mkwakwani, ambapo wanajangwani hao ndio mechi yao ya kwanza kucheza ugenini ndani ya michuano hiyo tokea ianze kupigwa msimu huu.

Droo ya kupatikana mechi hizo imefanyika saa 3.30 usiku huu katika Makao Makuu ya Azam Media, Tabata, jijini Dar es Salaam ambao ndio wadhamini wakuu wa michuano hiyo, ambayo imerejeshwa msimu huu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kukosekana kwa miaka kadhaa.

Azam FC na Yanga zinacheza ugenini baada ya kuingizwa kwenye kapu la timu zitakazoanzia ugenini huku Coastal na Mwadui vipira vyao vikichaguliwa kuanzia nyumbani, vyote hivyo akivichagua nahodha wa zamani wa Twiga Stars, Esther Chabruma, aliyestaafu kucheza soka mwaka huu.

Azam FC yatoa neno   

Mara baada ya droo hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, aliwashukuru waandaaji kwa kufanya droo ‘live’ huku akitoa masikitiko yake kwa TFF kuhusu tarehe waliyoipanga ya mechi hiyo, ambayo inaingiliana na mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance utakaofanyika Aprili 19, jijini Tunis.  

“Azam tuliomba hizi droo tangu hatua ya 16 bora kwa bahati mbaya sana hatukuzipata kwa kuwa watu walikuwa wakipanga chini ya meza na tulikuwa hatujui nani anacheza na nani na wapi, saivi tunashukuru kwamba iko wazi, lakini tunawaomba waandaaji wa mashindano waone ya kwamba hakuna droo inayofanywa katika nusu fainali, droo inafanywa kwenye 16 bora na sasa hivi ni hatua ambayo kila mmoja anajua anacheza na nani.

“Lakini kubwa zaidi tunasikitika tumesikia kwamba mechi ni tarehe 24 (Aprili), tukumbuke kwamba klabu zina majukumu ya mechi za Kimataifa (Azam na Yanga), isionekane kwamba ni wapinzani lakini tunasema hatuwezi kucheza mechi tarehe 19 Tunisia, tukafika hapa Aprili 22, tukaondoka kwenda Shinyanga Aprili 23 halafu tucheze na Mwadui Aprili 24. Hivyo tunaomba ipangwe ratiba kulingana na mechi zetu za kimataifa.

“TFF wapo hapa na wamesikia na waelewe hilo na tusionekane kama tunataka tafu kwenye mpira, vyovyote itakavyokuwa hiyo mechi inatakiwa isogezwe watu wacheze kwa ushindani, hatuwezi kusafiri kwa saa 14 halafu tuje hapa tusafiri saa nyingine mbili kwa ajili ya kucheza na Mwadui, wajipange na wajue kuwa hatupangi ratiba kwa kukurupuka, watu wajipange tutaweza kucheza tu, Mwadui ni ndugu zetu, rafiki zetu, tunawaheshimu na tumecheza nao mara tatu,” alisema Kawemba na kuungwa mkono na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, ambaye naye alipinga kwa upande wa Yanga watakaocheza na Al Ahly Aprili 20 jijini Cairo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, aliyekuwapo kwenye droo hiyo alisema hawaoni tatizo juu ya tarehe za nusu fainali na kudai asingependa kulizungumzia suala hilo mahali hapo.

Mabingwa hao Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), wamefika hatua ya nusu fainali baada ya kuichapa Tanzania Prisons mabao 3-1 huku Mwadui ikiichapa Geita Gold 3-0.

Yanga nayo iliipiga Ndanda mabao 3-1 ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku Coastal Union ikiichapa Simba mabao 2-1 jana, matokeo ambay yaliwashangaza wengi waliodhani itakuwa kazi rahisi kwa wekundu hao kuwachapa wagosi hao wa kaya.