WACHEZAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid Mussa na Himid Mao wako mbioni kuelekea barani Ulaya kusaka nafasi ya kucheza soka kulipwa.

Nyota hao wawili wanatakiwa na timu mbalimbali za Ligi Kuu, Farid akitakiwa nchini Ubelgiji na Himid ambaye ni kiungo mkabaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani anatakiwa nchini Denmark kwenda kujaribu bahati yake.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, amesema kwa sasa majina ya timu bado ni siri kwa kuwa bado wanaendelea na mazungumzo na timu wanazotakiwa kwenda.

“Awali Farid Mussa alitakiwa kuondoka mara moja kwa ajili ya majaribio hayo, lakini tumewaomba wenzetu wanaomtaka wamuache hadi amalizie mechi yetu ya pili dhidi ya Esperance na wamekubali, hivyo Farid ataondoka baada ya mechi hiyo,” alisema.

Kawemba aliongeza kuwa watatoa taarifa rasmi mara baada ya mchezo wa pili dhidi ya Esperance kuhusiana na hilo la Farid na pia kwa upande wa Himid anayekwenda Denmark.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, inatarajia kurudiana na Esperance Aprili 20 mwaka huu kwenye mchezo wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo mabingwa hao waliwapiga waarabu hao mabao 2-1 katika mechi ya awali iliyofanyika Uwanja wa Azam Complex jana.

Farid aliyekuwa kwenye kiwango bora, alifunga bao la kwanza la Azam FC huku Ramdhan Singano ‘Messi’ akitupia la pili na kuhitimisha ushindi huo.

Kama dili la Farid litafanikiwa basi ataungana na nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta, anayekipiga Genk ya Ubeligiji aliyojiunga nayo Januari mwaka huu akitokea TP Mazembe ya Congo DR.